MADAI  SITA (6) ENDELEVU YA WANAWAKE WANYONGE

Baadhi ya wanachama wa ushirika wa wanawake wavuja jasho Manzese “UWAWAMA” katika picha ya pamoja.

Sisi wanawake wavujajasho wa mjini na vijijini tunaojumuisha wafanyabiashara ndogondogo na wakulima wadogo, tumejumuika kimshikamano kusherehekea siku ya wanawake wavujajasho duniani leo tarehe 8/3/2022 katika ukumbi wa Amy Garvey  Manzese. Tukiwa  kama wanawake  tunaokumbana na madhila mbalimbali chini ya mifumo yote kandamizi, tunatambua kuwa maslahi yetu ni tofauti na maslahi  ya wanawake wa tabaka la juu. Kama ambavyo tuliamua kuanzisha jukwaa letu mbadala kusherehekea siku ya wanawake, baada ya mjadala mrefu   kupitia jukwaa hilo tumeazimia mambo sita yafuatayo kuwa madai endelevu ya wanawake wavujajasho.

  1. Tunataka uhuru kamili wa kiuchumi.

Licha ya kuwa na kampeni nyingi za kuwawezesha wanawake kiuchumi, kundi kubwa la wanawake wavujajasho wameishia kuwa watumwa wa taasisi za kifedha. Badala ya kuwezeshwa, tumeishia kufungwa minyororo ya madeni inayotuzidishia umaskini. Hii ni kwa sababu suluhisho linalotolewa dhidi ya hali duni ya kiuchumi kwa wanawake linastawisha zaidi mfumo kandamizi wa kiuchumi kuliko kuwakomboa wanawake.

Kampeni nyingi za kuwawezesha wanawake kiuchumi zinazinufaisha taasisi za kifedha zaidi kuliko kutukomboa sie.  Kupitia kampeni hizo tunahamashishwa kujiingiza kwenye  mikopo ya kinyonyaji, na kuwa wabinafsi kiasi cha kufanya chochote ili kufanikiwa ikiwemo  kuwanyonya na kuwakandamiza wanawake wengine. 

Sisi wanawake wavujajasho tumechoka kuwa watumwa, hivyo hatutaki tena hadaa za kampeni zisizo na manufaa kwetu. Kwa kauli moja tumeamua kuwa tutaendelea kupambania  uhuru kamili wa kiuchumi, na  tunataka ifahamike kuwa uhuru huo hauwezi kupatikana ikiwa kundi kubwa la wanawake litaendelea kutumikishwa na taasisi za kifedha. Hivyo tutatendelea kupambana na taasisi kandamizi za kifedha na dhidi ya mifumo yote inayozalisha matabaka ya kiuchumi hadi pale ambapo wanawake wote na tabaka zima la wavujajasho watakapokua huru. 

  1. Uhuru  wa kumiliki ardhi na ulinzi dhidi ya uporaji wake.

Sisi wanawake wavujajasho ndio wazalishaji wakuu, kwani asilimia kubwa ya wakulima wadogo vijijini na wafanyabiashara ndogondogo mijini ni wanawake na ardhi ndio nyenzo kuu tunayoitegemea.  Mfumo dume unatunyima haki yetu ya kumiliki ardhi kwa sababu ya jinsia yetu, na mfumo wa kibepari unatupora haki hiyo sisi pamoja na wanaume wavujajasho kwa sababu ya tabaka letu kiuchumi. Kwa sababu ya ubepari, wakoloni mamboleo wamepewa jina la wawekezaji na kukingiwa kifua na dola wapore ardhi yetu. 

Kila muda serikali inapotangaza ujio wa wawekezaji katika maeneo yetu, tunajawa wasiwasi na simanzi kwani kwa uzoefu wetu hatuna cha kutegemea zaidi ya kupoteza makazi na maeneo yetu ya uzalishaji mali. Siku zote tunaambiwa kuwa wawekezaji wanakuja kutuletea neema,ustawi na maendeleo, lakini ukweli na uzoefu umeonesha kuwa huja kutuangamiza kwa kutunyang’anya ardhi yetu ambayo ni nyenzo kuu ya uzalishaji mali na kutugeuza vibarua katika mashamba au viwanda vyao.

Wengine huja kama wawekezaji na kisha kutukodishia ardhi yetu wenyewe baada ya kuipora kutoka kwetu. Baada ya kuzipora ardhi zetu huishia kuziwekea uzio bila hata kuzifanyia shughuli yeyote ya kiuzalishaji. Iwe vijijini tunapoporwa mashamba au mijini yanapotwaliwa maeneo yetu ya biashara, wavujajasho wote kilio chetu hufanana.

Kwa kauli moja madhubuti tunasema tumechoka kugeuzwa watwana katika ardhi yetu wenyewe, na kuwa wazalishaji wasio na chakula wala mahitaji mengine muhimu kwa sababu ya kuporwa ardhi. Kwetu sisi ardhi ni utambulisho, urithi na uhai wetu, hivyo hakuna jambo muhimu kama kupigania uhai wetu. Hakuna haki yeyote muhimu kushinda haki ya kuishi, na kututenganisha na ardhi yetu ni kupora uhai wetu. Hivyo tutaendelea kudai haki hiyo na kupambana na uporaji katika sura na namna zake zote.

  1. Tunataka huduma za kijamii zilizo bora na  zitolewe bila malipo kwa wote.

Katika mfumo huu dhalimu kila kitu kimefanywa bidhaa ya kuuzwa sokoni ikiwemo huduma muhimu za kijamii kama afya, elimu, maji safi na salama n.k. Kwa kuwa mfumo wenyewe umetengeneza matabaka ya walio nacho na wasio nacho, kundi kubwa la wasio nacho linashindwa kumudu kupatia huduma hizo kwa sababu ya kukosa fedha. 

Linapokuja swala la ubaguzi katika huduma hizo, sisi wanawake wavujajasho ndio wahanga wakuu. Sisi ndio ambao hupoteza maisha kwa kushindwa kupata huduma bora za afya wakati wa uzazi kwa kuwa hatumudu gharama aghali katika hospitali zitoazo huduma bora ambazo nyingi ni binafsi. Hata tunapokwenda katika hopitali za serikali bado zinahitaji malipo na manunuzi ya vifaa vya kujifungulia  ambavyo pia huuzwa kwa bei ya juu. Huduma za kujifungua huanzia gharama ya kiasi cha shilingi elfu sabini na tano (75000/=), laki mbili (200,000), mpaka milioni tatu (3,000,000/=) kulingana na aina ya hospitali na namna ya kujifungua (kujifungua kwa njia ya kawaida au operation). Gharama hizo ni tofauti za gharama za kununulia vifaa vya kujifungulia. Kiufupi katika mfumo huu  tunanunua watoto wetu wenyewe,  wanawake wavujajasho tumekua katika hatari zaidi ya kupoteza maisha yetu ama ya watoto wetu wakati wa kujifungua.  

Eneo la afya ni sehemu ndogo tu inayoonesha namna ambavyo tunaishi katika jamii inayotweza utu kwa kuuza huduma. Kwa kuwa bila huduma hizi hatuwezi kuishi wala kuleta maisha mapya duniani kwa usalama, kwetu sisi haki za wanawake haziwezi kukamilika ikiwa haki ya kujipatia huduma hizi muhimu inatubagua sisi na tabaka zima la wavujajasho. Tumechoka kuishi kwa mashaka ya kupoteza uhai wetu na wa wanetu, hivyo tunataka mfumo ambao utu wetu utapewa kipaumbele kuliko fedha.  

  1. Tunataka haki-jiji kwa wote bila ubaguzi. 

Sisi wanawake wavujajasho wa mijini tunategemea kujipatia vipato vyetu kwa kufanya biashara ndogo ndogo katikati ya miji. Utegemezi wetu katika biashara hizo unatokana na kuwa wahanga wa uchumi ulioshindwa kulinda rasilimali zetu na kulimbikiza nyenzo za uzalishaji mali kwa wachache.

Uchumi ambao umeshindwa kujikita katika uzalishaji na hivyo kuishia kutengeneza taifa la wachuuzi.  Miongoni mwetu tumo wahanga wa uporaji wa ardhi uliopelekea kupoteza mashamba yetu, pamoja na kundi kubwa lenye uwezo wa kufanya kazi za uzalishaji viwandani ambalo halina ajira kwa sababu ya ukosefu wa viwanda. Hivyo chaguo pekee tulilo nalo ni kufanya biashara hizo za uchuuzi, na hatuwezi kuzifanya katika maeneo ambayo hayana wateja kwani mahitaji yetu yote yanategemea biashara husika.

Mbali na kutegemea biashara zetu, sisi pia ni watoa huduma wakubwa katika miji kwa watu wa matabaka yote. Sisi ndio wafanya usafi na wapishi katika maofisi na maeneo mengine ya miji. Kiufupi, shughuli zote za watu wa tabaka la juu katikati ya miji zinategemea huduma zetu kwa namna zote. Hata hivyo, swala la kuishi na kufanya shughuli zetu za kujitafuta kipato katika miji hii limeendelea kuwa huruma ya watawala na sio haki inayotambuliwa wala kuheshimiwa. Sisi wanawake wavujajasho pamoja na wanaume wa tabaka la chini tumekua tukipewa majina na kashfa za kuhalalisha unyanyasaji, udhalilishaji na uporaji tunaofanyiwa unaombatana na kuondolewa katikati ya miji kikatili. 

Kwa kuwa miji hii inajengwa kwa jasho letu kupitia kodi pamoja na shughuli mbalimbali tunazofanya katika ujenzi na ustawi wa miji hii, tunataka haki yetu ya kukaa na kufanya shughuli zetu katikati ya miji. Tumechoka kunyanyaswa na kuporwa mali zetu kwa kisingizio cha usafi na mipango miji. Hatukubali kuwa raia wa daraja la pili katika miji ambayo inastawi kwa jasho na nguvu zetu, hivyo tunataka mamlaka husika zipange miji kwa kuzingatia mahitaji ya wananchi wote bila ubaguzi.  Kama wahanga wakuu wa upangaji wa miji unaobagua kundi kubwa la wakazi wake, tutaendelea kupigania “haki-jiji” kwa wote bila ubaguzi hadi pale mapinduzi ya kusimika mfumo wenye usawa kamili yatakapopatikana. 

  1. Tunataka ajira zenye staha kwa wote.

Sisi wanawake wavujajasho tunatambua kuwa tatizo la ajira ni la kimfumo, na halitokani na  uzembe au ukosefu wa ubunifu wa mtu binfasi kama ambavyo tunaambiwa. Tunatambua  mahusiano ya uzalishaji mali yamesukwa kwa namna ambayo  kundi kubwa  la watu wenye uwezo wa kufanya kazi linakosa ajira na kugeuzwa watumwa wa  kundi dogo linalohodhi nyezo za uzalishaji mali. Na kuwa utumwa huo hustawi zaidi pale ambapo kundi la wasio na ajira huwa kubwa zaidi.  

Kama wanawake wavujajasho tunaathirika pia na tatizo hilo, kwani  tunawasomesha vijana wetu kwa tabu kupitia biashara ndogo ndogo na kilimo.  Wakati mwingine tunalazimika kuuza kila tulicho nacho ili kumudu kuwapatia elimu hiyo ambayo pia ni bidhaa katika mfumo huu. Hata hivyo baada ya yote hayo vijana wetu hurudi na kuendelea kuwa tegemezi kwetu kwa sababu ya ukosefu wa ajira. 

Kama wahanga, tunapinga dhana zote potofu zinazojaribu kuficha udhaifu huu wa kimfumo. Tuanakataa dhana zote zinazowalaumu wahanga kwa kushindwa kupata ajira ikiwa mfumo wenyewe dhalimu ndio umeshindwa kuzalisha ajira husika. Kwa mshikamano na vijana wetu tutaendelea kupambania ajira zenye staha, na kutaka kila anayefanya kazi afaidi matunda ya jasho lake. 

  1. Tunataka kutokomeza ukatili wa kijinsia katika sura zake zote.

Sisi wanawake wavujajasho ni wahanga wakubwa wa ukatili wa kijinsia. Kutokana na mfumo dume tumekua tukipitia vipigo, manyanyaso, pamoja na udhalilishwaji wa namna malimbali.  Tunatambua kuwa wanawake wote wanapitia ukatili huo, ila ni ukweli usiopingika kuwa sisi ni wahanga zaidi. Kutokana na ugumu wa maisha unaosababishwa na ubepari, wanawake wavujajasho huathirika zaidi na ukatili wa kijinsia , kwa sababu sisi ndio wahanga wa msongo wa mawazo na hasira za wanaume zinazotokana na ukali wa maisha.  Na kutokana na ukweli kwamba kila kitu kinahitaji fedha, hali zetu kiuchumi zinatunanyima fursa ya kuvifikia vyombo vya utoaji haki pindi tunapopitia ukatili huo. 

Kutokana na ukweli huo, tutaendela kupambana kutokomeza ukatili wa kijinsia, na kubwa zaidi kuendelea kupigania usawa kamili wa kijinsia. Usawa ambao tunaamini kuwa utapatikana pale ambapo mifumo yote kandamizi itavunjwa na kusimikwa jamii yenye usawa kamili inayoheshimu utu wa kila mtu.

Hivyo basi tumeamua;

(a.) Sisi wote tuliohudhuria leo tutaendelea kuunda vyombo mbadala vya  kuwaunganisha wanawake wavujajasho popote pale walipo ili kupaza sauti kwa pamoja kupigania madai hayo.

(b) Tutaendelea kutumia vyombo hivyo kuwafikia wanawake wengine wavujajasho na kuwahamasisha kuunganisha nguvu katika kupigania madai yetu. 

(c) Tutaendelea kujielimisha na kujenga uelewa wa kitabaka baina yetu na wanaume wavujajasho ili kuunda mshikamano imara utakaotuwezesha kuleta mapinduzi ya kimfumo na kujenga jamii yenye utu, haki na ustawi kwa wote.

Haya ni mapambano ya kuikumbusha jamii  kuwa madai ya wanawake yanatofautiana kulingana na matabaka ya wanawake husika. Madai haya endelevu ni kwa ajili ya wanawake wavujajasho na jamii nzima ya tabaka la wanyonge, na sisi wanawake wavujajasho tutaendelea kutimiza wajibu wetu kwa kuongoza mapambano ya kupigania madai haya.

Leave a Reply

Fill in your details below or click an icon to log in:

WordPress.com Logo

You are commenting using your WordPress.com account. Log Out /  Change )

Twitter picture

You are commenting using your Twitter account. Log Out /  Change )

Facebook photo

You are commenting using your Facebook account. Log Out /  Change )

Connecting to %s

SAUTI YA UJAMAA

Welcome to the Socialist Voice

Discover WordPress

A daily selection of the best content published on WordPress, collected for you by humans who love to read.

The Daily Post

The Art and Craft of Blogging

WordPress.com News

The latest news on WordPress.com and the WordPress community.

%d bloggers like this: