Kuhusu J.P.M na utawala wake,haya hayapaswi kupuuzwa.

Moja kati ya picha za hayati J.P.M siku za mwisho za uhai wake.

Nianze kwa simulizi ya mazungumzo baina yangu na rafiki wangu mmoja na mshirika wa kifikra katika  umajumui wa Afrika ambaye kwasababu kadhaa si miongoni mwa watu wangu wa karibu kwa sasa.

Kwa njia ya simu asubuhi moja majira ya kiangazi 2015 nikielekea shamba yeye akiniarifu kuwa alikuwa mkoa mmoja huko kanda ya ziwa nalizungumza naye na ninanukuu sehemu ndogo ya mjadala wetu;

Mimi:Sasa mdogo angu kwa hali iliyopo  katika CCM unadhani hata J.P.M kupita kutabadilisha nini,chama chenyewe kimeoza hiko,kila mtu mwizi mwizi tu.

Yeye:Ni kweli baharia,Ila unajua nini? inahitajika mtu aliye mzalendo ili mambo yaende mi naamini J.P.M anaweza kubadilisha hali.

Mimi:Ok,mi si-doubt commitment yake, concern yangu ni kuwa hayo mambo atafanya peke yake?,kama sivyo atafanya na nani na CCM yenyewe ndo hiyo. Afu hao jamaa wa UKAWA na wenyewe sio mzaa unaweza kukuta Dr.Slaa ndo akashinda na J.P.M na CCM yake wakashindwa.

Yeye:”Mwanangu baharia mi nnachojua mshua ni mwanaharakati wa maendeleo”.Sijui sana hizo siasa za vyama na sijali sana baharia.

Mimi:”Haaya,ila unajua huko aliko ni kugumu sana hasa hao wanachama wa chama chake hao,wengi wezi-wezi sana”.

Yeye:”True, baharia Ras lakini mi naamini atakomaa”.

Yakajiri yaliyojiri hata J.P.M “akashinda” Urais dhidi ya Edward Lowasa na si Dr.Slaa.Novemba 4,2015 nikiwa kijijini Lulanda,Mufindi yeye akiwa Dodoma nikizungumza  naye tena kwa njia ya simu,ninanukuu tena sehemu ya mjadala wetu.

Yeye:”Oi baharia si tupo huku kushuhudia zoezi la kesho”

Mimi:”Naelewa mdogo angu,sema,jambo la muhimu ni kujifunza kutoka katika uzoefu wa hao jamaa waliopita ambao wanasifika kwa skendo za wizi na ufisadi kisa kuna mwavuli wa kuwakinga juu yao,ntaku-mind sana kama na wewe utakuwa jizi na fisadi kama hao jamaa waliopita hata kama sitakuwa na uwezo wa kukufikia nitaku-mind kinoma”.

Yeye:Huku akicheka,”usiwaze baharia tutajitahidi man,kikubwa tuombeane”.

Sote hatukujua yatakayokuja mbeleni,ila sote tukashuhudia utawala wa J.P.M toka Novemba 5,2015 mpaka ulipotamatika Machi 17,2021 kwa kifo chake.Mazungumzo yetu kuhusu maoteo na matarajio kwa J.P.M yakaisha na sote mimi na yeye,yeye akiwa karibu na mie mbali kabisa tukashuhudia J.P.M akiitawala Tanzania.Sijajua mafunzo aliyojifunza toka kwa J.P.M  na ninatamani siku moja nijadili naye nipate kuyafahamu.

Mie nina mambo  ambayo nitayayasema kuhusu miaka 5 na ushehe ya utawala wa J.PM ambayo mimi nimejifunza na kuyaelewa kama alama za mafanikio au zinazopaswa kushadadia mafanikio.

Mosi;Kuutambua udhalili wa “utabaka” katika taifa.

Mara nyingi wengi wanaonadi “mafanikio” ya autawala wa J.P.M hujadili/orodhesha masuala yahususuyo vitu kama miundombinu mfano bwawa la umeme la Mwl.Nyerere ,reli ,vituo vya mabasi,viwanja vya ndege,barabara n.k kama mafanikio yake.Ilhali wakosoaji wake wengi wakijadili juu ya “ukali na/ama ukatili” wa dola dhidi ya kwa waliopishana naye fikra na mwendo wa utawala.Mimi nitajadili kuona ziada ya yatarajiwayo kusemwa kuhusu J.PM na/ama utawala wake wake.

J.P.M alijua na kukubali kuwa taifa letu limeundika  katika mfumo wa kitabaka hivyo kinyonyaji ambapo tabaka la juu limekuwa likisadiwa na tabaka tawala(linaloundwa na watu wa tabaka la juu) kuendeleza unyonyaji, uporaji ,fedhuli dhidi ya watu wa tabaka la chini na umehalalisha kiasi ambacho madhila ya watu wa tabaka la chini yana-asiliwa(naturalized),kukawaidishwa(normalized) na kupuuzwa (disregarded).

J.P.M alijitahidi kuona uwepo wa hilo na kujitahidi kwa namna yake kurejesha staha na utu wa watu wa tabaka la chini. Alifaulu ama hukufaulu, historia itampa alama/maksi na kumtetea ama kumuangamiza kupitia walioguswa(kwa uchanya na hilo).Mimi nashuhudia kuwa alilitambua hilo, akalikubali na akajaribu kufanya jitihada kwalo.

Huwenda wengine wakalidogosha hili ama kulipuuza ila kwa mawazo yangu kwa “makabwela” kama ambavyo watu wa tabaka la chini waliitana zamani hii ndio ilikuwa sababu ya kuiunga mkono TANU na viongozi wake  nyakati za kudai uhuru kwa kuwa tabaka la juu la wakoloni liliwanyonya na kuwapuuza makabwela huku TANU ikijipambanua na kuahidi kurejeshea staha zao zilizopuuzwa.

Yeye(J.P.M) alijaribu kutowapuuza makabwela wa karne 21 na wakati mwingine kuwalinda katika zama ambazo haionekani kuwa ni jambo la maana sana ama la lazima.

Najua kukubali “uwepo wa matabaka” na “mapambano ya kitabaka” si jambo moja na sikusudii kufanya uchambuzi wa kitabaka(class analysis) hapa ila nikusudiacho ni kujaribu kuonesha maamuzi ambayo yaliweza kuibua ahueni(concession) kwa tabaka linalopuuzwa na kunyonywa kwa namna ya adili(moral) na kushikika(material).

Kwa kukubali kuwa wezi na mafisadi wapo katika chama chake ilipaswa kuwasaidia watu wa tabaka la chini kuelewa kuwa huwenda hakuwa J.P.M hakuwa mwanachama wa chama kile(CCM) bali kingine(ambacho hakipo katika sajili za mamlaka),kuendelea kulisisitiza hilo katika khutba zake nyingi yawezekana ulikuwa ni wito kwa watu wa tabaka la chini kuwa hawana chama kinachojipambanua kama taasisi kulinda  maslahi yao hivyo kusalia kwao(survival) kutategemea wao kuwa na vyombo vyao imara vya kuwalindia maslahi yao na si mtu kama yeye ambaye licha ya jitihada zake aliwahimiza wazi kuwa anajua  akiondoka yeye yatarudi yaleyale, maana yake hakukuwa na salama kuikabidhi hatma yao kwake(J.P.M).

Ukiwa Kilosa, Mvomero na ukawauliza wakulima na wazalishaji wengine wadogo kuhusu masuala ya uporaji ardhi watakufunza vema hili ama wachuuzi wadogo mijini almashuhuri “machinga” wana cha kusema kwa kina  juu ya hoja hii.

Pili, Ukweli kuhusu nafasi ya Tanzaia kimataifa.

Alitukumbusha kuwa Tanzania na Afrika si muamuzi katika duru za ulimwengu,bado hatupo katika ngazi hiyo.Pia mashirikiano ya kimataifa maana yake ni mahusiano baina ya mataifa kwa hiyo pahala ambapo hakuna mahusiano mema/tija hapana mashirikiano.

Hata kama hakusema kwa kauli ila alichukia kwa haiba mahusiano yasiyo haki na ya kinyonyaji baina ya taifa lake na mataifa mengine na ndio maana hakuwa “kipenzi (dear)” wa mataifa ambayo tunalazimishwa kuwa ni shuruti kuwa wapenzi nayo vinginevyo tutaangamia.

Dhahiri ya takwimu ni kuwa mahusiano baina yetu(mataifa ya kaskazini/yaliyoendelea na mataifa ya kusini/nchani/mkiani/yanayoendelea) ni ya kinyonyaji kwa miaka mingi, hivyo hata nafasi yetu katika  kinachoitwa mashirikiano baina yetu imekuwa ni sie “kujikomba”,”kushurutishwa na “kuombaomba” jambo ambalo linazidi kuukimbiza uhuru kiduchu tulionao wa kujiamulia.

J.P.M alilijua hilo, Ila kwa kuwa mizizi ya aina hiyo ya mahusiano ni imemea kustawi na kuwa  mirefu mno basi jitihada zake zilikuwa na ukomo(limited).Alama ni kuwa katika miaka 60 ya uhuru miaka ymitano (5) ya utawala wake(J.P.M) Tanzania ilikuwa na uwezo wa kusema  “hapana” dhidi  matakwa ya wakubwa ama wadogo ikiwa maslahi yake yaliwekwa rehani,ilifanya hivyo kwa kauli na matendo kadhaa ya kisera na hata katika  vipaumbele kwa shughuli za kiuchumi.

Hili pia linaweza lisichukuliwe kwa uzito, lakini bayana ni moja tu,mnaweza kujiita taifa pale tu mnapoimarika katika uhuru wa kujiamulia mambo yenu.

Hakuwa miongoni mwa watawala wa kiafrika ambao husombwa kwa makundi kwenda kuwasikiliza viongozi wenzao wa mataifa mengine,yaani viongozi zaidi ya 50 kusombwa kwenda  kumsikiliza kiongozi wa Marekani ama Ufaransa na siku hizi hata India na Israel.Hakuonekana kwenye mikumbo hiyo ambayo, wenye akili wanajua kuwa haiisaidia Afrika kwa lolote la maana.

Ni katika wakati wake ndipo wanyonyaji waliitwa mabeberu jambo ambalo lilikuwa si msamiati katika saiasa za nchi kwa miaka takribani 40, hili liliwakera walioitwa mabeberu pamoja na wale “waswahili” ambao wanadhani mnyonyaji akikupatia ‘makombo’ unapaswa kumpigia magoti na kumwita “mshirika”.Ni mfano wa kigezo cha diplomasia ya ukombozi katika zama za diplomasia ya uchumi(ambayo kimantiki na uzoefu wa hapa kwetu imekuwa diplomasia ya utegemezi na kujikomba wa mataifa yaliyopiga hatua)

Tatu;Ukali katika kulinda rasilimali za nchi.

Wakoloni na mabepari wamelifanya eneo letu hili(Tanzania na Afrika) kuwa pahala pa kukomba rasilimali na malighafi  kwa miaka mingi bila kuhojiwa na tukafika wakati tunawapa ushirikiano katika hilo.

Wamefanya hivyo isipokuwa katika kipindi cha  miaka  kadhaa baada ya uhuru wa Tanganyika na baadaye muungano wa Tanzania.Wamefanya hivyo kwa mgongo wa sheria na kwa uporaji wa mabavu/ujangili/ujambazi/ufisadi.

Jitihada za J.P.M katika kulinda rasilimali zilikuwa tofauti na watangulizi wake akiwamo Mwl.Nyerere kwa kuwa yeye amekuwapo katika nyakati hizi ambazo tumerushusu ushirika baina ya unyanyoji wa kimataifa na uporaji/ulanguzi/magendo/ufisadi wa ndani kwa kiasi kikubwa kushinda nyakati zote katika historia yetu hivyo katika jitihada zake alikumbana na upinzani mkubwa kuanzia ndani ya nchi.

Hata yale yaliyopigiwa kelele na wadau mbalimbali kuhusu wizi na uporaji wa rasilimali alipojaribu kuyarekebisha alipata ukinzani kutoka hata kwa wadau wale walioyapigia kelele.

Kwa kuwa wengi katika waporaji wa ndani walikuwa katika tabaka tawala hasa katika chama chake cha CCM, wakora hao walikuwa katika nafasi nzuri ya kujua pa “kuminya” ili kudhohofisha jitihada za mageuzi katika ulinzi wa rasilimali  na kuyatumia vema makosa ya maamuzi yake mbalimbali kwa manufaa yao huku wakiibua hoja na kuzinadi kuwai wanawapigania “wanaoonewa na kuteswa”

Alijitahidi kutukumbusha mara zote kuwa mustakabali wa ustawi wetu unapaswa kuamuliwa na sisi wenyewe kwa kutumia rasilimali zetu na sio “wawekezaji”  ama mataifa yenye nguvu, hukuwahi kusema “tunawahitaji wao zaidi kuliko wanavyotuhitaji sisi”.

Hivyo ndivyo mimi nilivyomuelewa,ila kwa kuwa mtu yule alikuwa wa “toleo la tofauti” huwenda na mie pia sikumuelewa kama ambavyo wengi hawakumuelewa na wakampima kwa mizani yao ya kinadharia(ideologies) kisha wakaishia kutumia nadharia wanazozipinga kila siku ama kumkosoa.

Nimepita mijini na vijijini nimekutana na wengi mno wenye kumpenda  na kuhitaji uwepo wake, siamini kama wanafanya hivyo kwasababu ya daraja la juu la Kijazi la Ubungo au reli ya SGR, naendelea kujifunza wanachokikosa kwa kukukosa.

.

Muhemsi Mwakihwelo ni mwananchi wa Tanzania na makala haya mawazo na maoni yake binafsi wala si msimamo wa wavuti yetu, tumeyanakili mala haya kutoka katika ukurasa wake wa mtandao wa Facebook

Leave a Reply

Fill in your details below or click an icon to log in:

WordPress.com Logo

You are commenting using your WordPress.com account. Log Out /  Change )

Twitter picture

You are commenting using your Twitter account. Log Out /  Change )

Facebook photo

You are commenting using your Facebook account. Log Out /  Change )

Connecting to %s

SAUTI YA UJAMAA

Welcome to the Socialist Voice

Discover WordPress

A daily selection of the best content published on WordPress, collected for you by humans who love to read.

The Daily Post

The Art and Craft of Blogging

WordPress.com News

The latest news on WordPress.com and the WordPress community.

%d bloggers like this: