Tarehe 9 Desemba. Sisi wavuja jasho tusherehekee nini?

Picha kwa hisani ya mtandao.

Na, Muhemsi Mwakihwelo

Kwa kuwa, hakuna kisichobadilika isipokuwa mabadiliko yenyewe basi ni haki kwetu kujumuisha kuwa hata wasingekuja hapa nchini kwetu wamishonari, wapelelezi na wafanyabiashara kutoka mataifa ya Ulaya(hasa Ulaya magharibi) nchi yetu isingesalia vilevile kama ilivyokuwa katikati ya karne ya 19.

Ni ngumu kutoa taswira sahihi ya nini kingejiri na ni hatari kugeukia katika “uaguzi”, ila bayana ya kisayansi ni kuwa,lazima iliyokuwa Tanganyika isingesalia vilevile hata kama wakoloni wasingeipora kwa Wenyeji wake. Hivyo basi Tanganyika/Tanzania “kutosalia vilevile” si muujiza unaopaswa kutumiwa na “mashabiki” wa watawala kutaka “kuwazima” wale wenye kufikiri ama hata kudhani hatustahili kuwa hapa(ngazi tuliopo kiustawi).
Yanasemwa mengi lakini mie kwa udogo wangu “kijamii” nitataka nifikiri na kudadisi kuwa tunapoelekea kusherehekea miaka 60 ya uhuru wa Tangayika,yatutosha kufurahi kwa kivuli cha kauli kuwa moja tu kuwa “tumetoka mbali na hatukuwa hapa miaka 60 iliyopita”?
Nitajadili kwa jicho la anayeitwa “mtanzania wa kawaida”,nitajadili kwa jicho la anayeitwa “mnyonge”,nitajadili kwa jicho la anayeitwa “mvuja jasho”.
Nikikopa hekma ya mtu mashuhuri kushinda wote Tanzania(kwa maoni yangu),Julius Nyerere ambayo aliibainisha wakati akihutubu katika mkutano na wafanyibiashara wa kitanzania mwaka 1989 alipohoji ju ya umaana na tija ya maonesho ya silaha,zana na gwaride za kijeshi katika sherehe za “kitaifa”.

Kwake yeye (Nyerere) aliona kuwa kufanya hivyo kwa muktadha wa Tanzania tija yake ni kiduchu na ni Sawa na kusherehekea umaridadi na ustadi wa watu wa mataifa mengine yanayounda zana na silaha hizo za kijeshi ambazo sisi huzinunua tu kwao.Sidhani kama hilo limebadilika sana leo,ila hoja ya msingi hapa ni nini tumekuwa tukikisherehekea?

Ni kweli tunaitwa taifa huru, tuna kiti/viti katika jumuiya za mataifa na tunao watu wanaotutawala hapa ambao ni Watanzania kama sie,lakini akisi ya uhuru kwetu tuipime kwa hayo tu ya kiutawala/kutawaliwa.Watawala wetu sasa si wazungu na wengi wana ngozi za miili zinazofanana na sie, lakini tarehe 9 Desemba ikiwa tutakwenda katika viwanja vilivyotengwa kwaajili ya magwaride ya kijeshi ambako huko “wakuu” wa nchi watahudhuria, tutakalolifurahia ni lipi hasa baada kutawanyika viwanjani “wakuu” watakapokwenda katika dhifa za kitaifa na wananchi wa kawaida kuelekea majumbani mwao?

Labda kujibu hayo mmoja atapaswa apitie mambo kadhaa yanayojadili ni kwanini tuliudai uhuru wenyewe,zipi zilikuwa hamasa na ahadi za kutafuta uhuru na yapi yemejiri kwa wavuja jasho baada ya uhuru, yenye kuakisi ahadi na hamasa za kudai uhuru. Ni Haki kusema wakoloni ni waovu ,wabaguzi, wanyonyaji,na wakandamizaji, na natumai ni watu wachache mno wanaweza kulipinga hilo.

Lakini mwenge wa uhuru uliposimikwa mlima Kilimanjaro lengo lilikuwa ni ishara kuwa nuru yake(mwenge) iangaze ndani na nje ya mipaka Yetu Hii tuliyopangiwa na wakoloni,ilete nuru kulikokuwa giza,irejeshe tumaini palipokuwa na dhalili n.k na mwenge ule hukimbizwa nchi nzima tena ukiyanukuu maneno hayo hayo.

alxander-gwebe-nyirenda

Alexander Gwebe Nyirenda akisimika bendera ya Tanganyika katika kilele cha mlima Kilimanjaro. Picha kwa hisani ya mtandao

Baadaye azimo la Arusha likanadi usawa wa binadamu, na kuainisha kuwa tulionewa,kupuuzwa na kunyonywa kiasi cha kutosha sababu ya unyonge wetu na kuwa tunataka mapinduzi ili kuondokana na madhila hayo.

Tarehe 9 Desemba itapofika halafu tukawatizama watanzania kwa wingi wao na makundi yao ya kijamii hasa yale ya shughuli zao za kiuzalishaji/kiuchumi(acha yale makundi yanayoweza kuwa ya kiubaguzi kama dini,kabila n k) je,tunaweza kuonesha mapinduzi hayo yaliyoahidiwa na Azimio la Arusha bila mashaka?
Yaani mkulima mdogo huko kijijini na mchuuzi katika jiji(machinga) wanapaswa waseme “tulionewa” kiasi cha kutosha ama waseme “tunaonewa” kiasi cha kutosha?Wafugaji wanaoporwa ardhi na vijana wasio na ajira zenye staha wanapaswa waseme “tulipuuzwa” kiasi cha kutosha au “tunapuuzwa” kiasi cha kutosha? Wachimbaji wadogo na wakaazi wanaozunguka maeneo yenye rasilimali madini hasa yenye uwekezaji mkubwa wa mabepari,wanapaswa waseme “tulinyonywa” kiasi cha kutosha au “tunanyonywa” kiasi cha kutosha? Sherehe za uhuru wa Tanganyika ni “sherehe za watanzania” ama sherehe za “serikali ya/za Tanzania”?

Hali ya kutokuwepo vurugu katika nchi hii ni jambo jema mno na wote, “watanzania wa kawaida” na “watanzania wasiokuwa wa kawaida” linatufaidia,ila je,hiyo si matokeo ya jitihada za watanzania wote?, mbona taswira iliyopo ni kanakwamba hilo ni matokeo ya jitihada za watanzania wasiokuwa wa kawaida pekee?

Imesimuliwa na imeandikwa kuwa wakoloni walitutawala bila idhini yetu na hawakutegea sikio mawazo, hisia na hamasa zetu isipokuwa kufanya jitihada za kuneemesha mataifa yao kupitia makampuni yaliyokuwa yakipoka waziwazi rasilimali zetu, wazee wetu walifadhaika sana.Wakoloni wale walipotaka kujipunguzia mzigo wa gharama za utawala waliibua kodi(tozo) mbalimbali ambazo hazikuheshimu ridhaa na idhini ya watanganyika wakati huo.

Je,kufika Desemba 9, “wananchi wa kawaida” wanaohimizwa kufurahia uhuru, wanao uhuru wa kuamua juu ya kodi na tozo wanazotozwa,ama la serikali ni torati kwao na asiyetaka ahame nchi? Je, nani ana udhibiti rasilimali kama madini,mazao ya misitu,mazao ya kilimo n.k,thamani yake katika mnyororo wa biashara na uzalishaji vinaakisi hali ya “wananchi wa kawaida(wazalishaji)” kiasi cha wao kujiridhisha kuwa kweli wakoloni hawakuwa na maana ila watawala wa sasa wastahiki heko?

wachimbaji wadogo ishinabulanda

Wachimbaji wadogo Ishinabulanda,Shinyanga. Picha kwa hisani ya mtandao

Mfano,ukivaa viatu vya machinga(jambo ambalo kwa wengi wanaona ni upumbavu kulifanya) anayefukuzwa Mbezi na kupelekwa Kifuru unapata wakati mgumu kuelewa tofauti kati ya mkoloni mzungu aliyegawa Masaki na Oyster Bay kuwa ni eneo la wazungu, Upanga la wahindi na kwingineko ni la watu weusi na huyu mtawala wa leo asiye mzungu anayegawa Posta na Kariakoo kuwa pa wenye pesa na Kifuru na Kilungule pa wasio na pesa.Machinga huyu tarehe 9 Desemba itapofika asherehekee lipi?

Mwananchi anayeporwa ardhi pale Kiomoni na Mzizima ama Chongoleani kule Amboni yeye naye asherehekee nini Desemba 9,mwananchi huyu ambaye wazee wake waliletwa hapo Tanga na wakoloni kama manamba kutoka bara,leo anaporwa alichonacho na tena kwa lugha ileile aliyoitumia mkoloni kumteka mzee wake kwa mabavu(ya kiuchumi) na kumleta Tanga kama manamba, lugha ya kusema lengo ni “kuiletea maendeleo nchi”.

Hivyo licha ya “makelele na mbwembwe” za vyombo vya habari kupamba sherehe hizo,zipo sauti za mamilioni ya watu ambazo “hazi-enjoy” kama ambavyo wananchi wasiokuwa wa kawaida “wanavyo-enjoy”.
Hawa-enjoy kwakuwa dola letu Tanzania halijajiondoa katika mizani ileile ya dola haramu la kikoloni,linafanya unyapara vilevile dhidi ya wananchi wa kawaida na mbaya zaidi linasimama kama kikwazo kwa wavuja jasho wanapojaribu kujikwamua dhidi ya ukatili wa “dola na makampuni ya kinyonyaji ya nje” kutokana na mkondo wa mfumo na sera za uchumi

ambazo dola limezikumbatia, wavuja jasho katika kilimo,uvuvi,ufugaji,uchimbaji madini,sekta ya utoaji huduma,viwanda wanaachwa washindane na wenye maguvu bila kulindwa na kutetewa na dola letu.

Kwa kuwa makala haya si makala ya lawama bali ni makala ya kuonesha kuwa kinachoitwa sherehe za uhuru si sherehe za ki-taifa maana si wote watakaomudu ama kuwa na sababu ya kusherehekea.Uzalendo hauwezi kuwa ni matokeo ya sisi kwa kuwa nchi yenye vivutio na rasilimali nyingi, mfano ni dhana duni mno kudhani watu wanapaswa kujivunia Tanzania kwasababu ya uwepo wa mlima Kilimanjaro, Serengeti na Zanzibar ama kwasababu kuna madini ya Tanzanite.Tabia ya fahari kwa nchi itatokana na mahusiano sawia/tija baina ya “watu” kisha “watu na rasilimali” zilizopo(ardhi,madini,vivutio,njia za uzalishaji mali) n.k katika jitihada za kusaka ustawi wao.

Miaka ya nyuma angalau watawala waliona haya/aibu na kujibidiisha kujidhibiti na kutojitofautisha “ki-hali” na wanaowatawala kwakuwa tu wana “fursa” ya kufanya hivyo kupitia nyadhifa za utawala,leo watawala hawana haya/aibu wanalimbikiza mali,wanakoga katika anasa na neema kubwakubwa,kisha wanafanya himizo tushangilie uhuru pamoja nao, yaani asiyemudu mlo na anayesaza mlo wafurahie mafanikio pamoja, hakika huo ni wimbo mgumu kuuimba.

Muhemsi Mwakihwelo, ni mwananchi wa nchi ya Tanzania.
+25742185692
muhemsimwakihwelo@gmail.com
Itagutwa,Isimani-Iringa
20201

Leave a Reply

Fill in your details below or click an icon to log in:

WordPress.com Logo

You are commenting using your WordPress.com account. Log Out /  Change )

Twitter picture

You are commenting using your Twitter account. Log Out /  Change )

Facebook photo

You are commenting using your Facebook account. Log Out /  Change )

Connecting to %s

SAUTI YA UJAMAA

Welcome to the Socialist Voice

Discover WordPress

A daily selection of the best content published on WordPress, collected for you by humans who love to read.

The Daily Post

The Art and Craft of Blogging

WordPress.com News

The latest news on WordPress.com and the WordPress community.

%d bloggers like this: