Hoja Potofu Kumi na Tano Kuhusu Wamachinga

1. Wanakwepa/Hawalipi kodi

Machinga hulipa kodi, ada na tozo zote za serikali. Mosi, wanalipa Kodi ya ongezeko la thamani(VAT) wanunuapo bidhaa.

Pili, hulipa tozo zingine kwa mujibu wa sheria na sheria ndogondogo kulingania kima cha mitaji yao. Kipekee naona ndio watoa huduma zinazokidhi watu wenye kipato duni ambao wanafanya shughuli zao katikati ya miji.

Tatu,  Umachinga ndilo eneo lililo salia katika kukabiliana na changamoto ya ajira ambapo kiwango na uwezo wa kuajiri kwa sekta ya rasmi ni mdogo kuliko nguvu kazi iliyo tayari kuingia katika ajira.

2. Wamachinga wanafanya shughuli zao kiholela

Muwekezaji wa madini hupelekwa sehemu ambayo imethibitika kitafiti kuwa na madini husika. Basi dhana ya uholela wa Wamachinga ni kutoheshimu tu kuwa “uwekezaji” wa Machinga unafanyika zaidi katika mikusanyiko ya watu.

Kama ambavyo wawekezaji wengine huwekewa mazingira bora ya uwekezaji ikiwamo miundombinu na misamaha ya kodi ,kumbe kinachopaswa ni kuweka mazingira bora ya “uwekezaji” wa machinga ambao takwimu zinaonesha ndio uwekezaji mkubwa unaoajiri watanzania wengi nyuma ya kilimo.

Hakuna uholela, isipokuwa hakuna mazingira mazuri ya uwekezaji ikiwamo kutengewa na kujengewa mabanda mjongeo katikati ya Jiji, vituo vya mabasi n.k. Pembeni ya miji hakufai kwa “uwekezaji” wa umachinga.

3. Wanasababisha msongamano jijini  na kuziba njia za watembea kwa miguu.

Ni muhimu ijulikane kuwa kwa sehemu kubwa Machinga wanategemea watembea kwa miguu kama wateja wao wakubwa.

Kwahiyo hoja hii ina matobo, aidha ina zungumzwa na watu ambao sio watembea kwa miguu, inawatumia watembea kwa miguu kama sehemu ya kuficha uhalisia au mitazamo yao au hofu zao kuhusu Machinga.

Pili, zipo sababu zingine zinazoweza kusababisha foleni au msongamano au kuzibwa kwa njia za watembea kwa miguu ambazo zina mchango mkubwa kuliko Umachinga kama vile; Uwingi wa magari madogo na maegesho yao yasiyo sahihi, wembamba wa njia au kupita kwa watembea kwa miguu kutokana na majengo ya migahawa au maduka makubwa na stores kusogezwa zaidi karibu na barabara, Udogo wa Stendi za mbasi ya Umma na kusababisha foleni ya kugombania magari na mipango miji kutozingatia sehemu kwa ajili ya shughuli za Machinga.

4.Wamachinga katika  ya jiji au miji husababisha matukio ya uhalifu.

Hakujawahi kutokea Siku katika ripoti za wataalamu wa masuala ya usalama wa raia(jeshi la polisi) wakatujuza kuwa uhalifu ni matokeo ya umachinga.

Kama ambavyo hatusemi siasa ni ufisadi kisa kuna mafisadi katika siasa ama dini ni utapeli kisa wamo matapeli katika dini ndivyo hivyo hoja ya kuhusisha “uwekezaji wa umachinga” na uhalifu inapaswa kupuuzwa na Kwa kuwa tuna vyombo vya sheria wahalifu wakashughulikiwe huko baada ya kuushitaki uwekezaji wa umachinga.

5. Wanachafua mazingira na kufanya jiji kuwa chafu.

Dhana hii ni dhana inayojaribu kuundoa ukweli kuwa  wachafuzi wakubwa wa mazingira ni wenye viwanda,ndio wenye kuzalisha taka sumu, hewa chafu, makelele makubwa n.k.

Wamiliki wa magari na vyombo vya moto pia ndio wachafuzi wakubwa wa mazingira.

Machinga hakati mti, hazalishi taka sumu, kelele zake ni stahimilivu hazalishi moshi, tunalo baraza la mazingira chini ya ofisi ya makamu wa Rais (NEMC) tukatafute huko nani mchafuzi mkubwa wa mazingira.

Wamachinga maeneo mengi’ taka wanazozalisha ni mabaki ya vifungashio vya bidhaa (karatasi na nailoni) ambazo ni rahisi kukusanyika na wengine hulipa tozo za usafi kwa halmashauri na hata kusafisha wao wenyewe maeneo yao ya kazi.

6. Machinga (watoa huduma za chakula) ni tishio au hatari kwa afya watumjaji wa bidhaa zao.

Dhana hii ni matokeo ya kasumba ya kuwaona wengine takataka/wachafu licha ya kuwa na mitaji kiduchu na vitendea kazi vichache na mazingira mabovu kiuwekezaji machinga wa huduma za vyakula hawana chaguo isipokuwa kuboreshanhuduma zao kwani wasipofanya hivyo wateja huwakimbia hivyo hufanya jitihada kutoa huduma bora ikiwamo usafi.

Licha ya hivyo tuna mabibi na mabwana afya wa mitaa ambao hutoza faini ama kuzifungia biashara zinazokiuka masharti na kanuni za Afya.

Watoa huduma hawa hutoa huduma si tu kwa Machinga wenzao bali watu wengi walioko katika shughuli zao ambao wengi hawana “ubavu” wa kwenda kupata huduma hiyo “Serena Hotel”.

7. Tishio kwa wafanyabiashara wakubwa na kati.

Dhana hii imeundwa katika msingi wa “uhodhi” isivyobahati na watu wanaopiga mnada wa soko huria.

Machinga hawazalishi bidhaa wanazouza,hawaagizi ama kuzifuata China,Arabu ama Ulaya ,wanazinunua Kwa wafanyabiashra hao wakubwa na wa kati na kuzisambaza kwa mlaji(mteja) wa mwisho.

Njama iliyopo ni wafanyabiashra wakubwa kudhibini na kuhodhi kwa kuivunja nafasi ya machinga na kulazimisha mteja ashughulike moja kwa moja na muhudho mkuu ilinapokwe hata uwezo wa kujadili(negotiate) bei.

Ni njama ya uhodhi inayotengeneza taswira ya machinga kuwa jitu lenye mabavu ya Uchumi Ilhali wengi ni wabangaizaji.

8.Wanauza au wanasambaza bidhaa haramu

Ni aina nyingine ya dhana chonganishi toka kwa wenye chuki na machinga.

Vyombo vyenye majukumu ya usalama vikimkamata mwanasiasa na silaha kinyume na sheria haviripoti kuwa wanadiasa wanamiliki silaha kinyume na sheria bali kitamuwajibisha muhusika na si kada yake,kabila,Dini ama tabaka yake.

Vyombo husika vishughulike na watengenezaji,waagizaji na wasambazaji wa bidhaa hizo haramu bila kuwahusisha na machinga kama wawekezaji.

9. Wanafanya shughuli zao kwenye mazingira hatarishi.

Kwa asili ya aina ya uwekezaji wao machinga takribani wote wanafanya kazi katika mazingira stahiki.

Hoja ni kuwa migodi yao(maeneo wanayofanyia kazi) hayaboreshwi kukidhi uwekezaji wao na bade eti kuna shaka juu ya uhalali wao(jambo la aibu kabisa).

Watawala wanapopangilia miji wanasahau aina za watumiaji miji na aina za shughuli zao hatma yake ,ubabe ulokozwa chuki inageuka mila ya watawala.

10. Kikwazo kwa haiba ya jiji lilostaarabika.

Hii ni hoja yenye fedheha kubwa kwamba tunapanga miji/majiji ambayo hayatusadifu wenyewe isipokuwa wachache katika Jamii.

Fikara ya ukoloni na ukaburu isiyo na tofauti na mabango ya “Blacks Only” na “Whites Only” kule Afrika Kusini na Marekani kwamba leo atika ya jiji kutafuta ridhiki ni  “Riches Only”  kisa tunataka “haiba ya Jiji”, Jiji ambalo ni letu sote.

Hii ni sawa mzazi anayemchukia na kumtimua mwanawe ambaye Yeye mwenyewe hakumtunza kisa mwanawe huyo sio tajiri na haleti “haiba” nzuri nyumbani.

Dhana hii ya kikaburu ni hatari maana imeundwa na watawala wakubwa kabisa nchini.

11. Hawawezi kujipanga na kufuata taratibu na sheria.

Dhana hii ya kuwajinaisha Wamachinga haina ukweli hata kidogo na ina ruka hoja hata inayoeleza juu ya makundi mbalimbali ya wamachinga.

Wapi Wamachinga wanaozungusha bidhaa zao majumbani mwa watu, wapi wanazo uza katika vyombo vya usafiri na wanaopanga biashara zao mahala pahala fulani. Hivyo hufanya shughuli katika maeneo ya umma hata binafsi mfano majumbani.

12. Wamachinga wanapanga bidhaa zao barabarani, kuzuia biashara za maduka makubwa na kusababisha ajali.

Tuna askari wa usalama barabarani, kati ya vyanzo vya ajali vinavyoanishwa hatujawahi kuambiwa hata mara moja kuwa ni machinga. Mara nyingi itasemwa uzembe wa madereva, ubovu wa miundo mbinu, ubovu wa vyombo vya usafiri na zaidi hali ya hewa hakuna ajali inayotokana na uzushi kuwa machinga wanapanga biashashara katikati ya barabara isipokuwa pembeni ya barabara mahala ambapo ndipo wanapaswa kufanya uwekezaji wao.

Barabara ni maeneo ya umma hivyo umma wote una maslahi nazo watembea kwa miguu,wafanyabiashara wakubwa na wadogo vilevile hakuna anayestahili kutolewa kafara hasa katika kusaka ustawi wa uchumi.

Tutizame haki za matumizi ya maeneo ya umma(access to public spaces),tutizame  haki jiji(right to city) kwa muktadha wa manufaa ya uchumi Kwa wote.

13. Si sehemu ya uchumi rasmi.

Ni jambo la haya mno kwa muktadha wa Tanzania kukumbatia hoja hii.

Ndo Kusema tunajaribu kutokijua kitu tunachokifahamu uwepo na tija yake.

Busara ni kurasimisha badala ya kujinaisha na namna ya kurasimisha ya kwanza ni kutowashambulia badala yake kuwaimarishia uwezo wa uratibu katika maeneo yao Ili kupitia vyombo hao(sio Hawa mapandikizi wa dola) waweze kuujenga utaratibu wa uendeshaji shughuli zao ikiwamo usafi n.k.

14.Wanapangwa hawaondolewi.

Wakati baadhi ya wakuu wa mikoa wakila kiapo kuhakikisha wanawakomesha Machinga, bado inaitwa kuwapanga.

Kuwapanga kunakohusisha kuondoa uhai mfano,  tukio la Vingunguti kuwapanga kunako husisha uvamizi wa usiku wa askari na walinzi wenye silaha, kuwapanga kunakowapeleka machinga nje ya mji mfano Kivule kwa Dar es Salaam.

Hili la kuwapanga ni mbadala wa Kusema kuwafukuza.

Halafu kama Kuna Eneo lenye tija kwa wamachinga wngekwishakwenda bila mtutu wa bunduki na uvamizi wa usiku, tafsiri ni kuwa serikali inafukuza machinga si kuwapanga.

15.Wanapewa uhalali ni wanasiasa.

Hoja hii si ya kisayansi.Ukweli ni kuwa machinga wanapewa uhalali na aina ya mfumo ulioligeuza taifa hili kuwa soko la bidhaa ukafubaza shughuli za uzalishaji mali ikiwamo ,kilimo na uzishaji bidhaa viwandani shughuli ambazo zingeweza kutoa ajira Kwa maelfu.

Matokeo yake ni vijana kusalia wachuuzi wa bidhaa za viwanda vya nchi nyingine.

Umachinga maana yake ukosefu wa ajira rasmi/zenye tija/zenye ulinzi.

Nafasi ya siasa ni kufanya maamuzi thabiti ya Mapinduzi Makubwa ya uchumi zaidi ya haya ya kufurahisha watalii na mabepari wawili watau huku ukiangamiza watu unaowajibuka kuwasaidia.

Leave a Reply

Fill in your details below or click an icon to log in:

WordPress.com Logo

You are commenting using your WordPress.com account. Log Out /  Change )

Twitter picture

You are commenting using your Twitter account. Log Out /  Change )

Facebook photo

You are commenting using your Facebook account. Log Out /  Change )

Connecting to %s

SAUTI YA UJAMAA

Welcome to the Socialist Voice

Discover WordPress

A daily selection of the best content published on WordPress, collected for you by humans who love to read.

The Daily Post

The Art and Craft of Blogging

WordPress.com News

The latest news on WordPress.com and the WordPress community.

%d bloggers like this: