Msukule wa “U-Tanganyika” na ibada ya sanamu kwa mkoloni.

Mwl.Julius Nyerere akishangilia uhuru wa Tanganyika akiwa amebebwa na wafuasi wake.
Picha kwa hisani ya mtandao wa GettyImages

Wavuja jasho lazima waelewe hayo ili wasihadaiwe na siasa za madaraka zenye lengo tu la kushika dola hilihili lenye sifa za kikoloni.Kulipa jina la Tanganyika ama Tanzania hakuliondolei sifa hizo,hivyo suluhu kwao si uwepo serikali ya Tanganyika.

Kwa zama nyingi kumekuwako na hulka ya watu kutaka/kutamani mapungufu,kushindwa ama uzembe wao uwe umetokana na watu ama kitu kingine na si wao wenyenyewe.Hulka hiyo ikikua basi hujiinua na kufikia ngazi ya juu yaani hata kama hakiko kitu ama mtu ama jambo lenye kuhusika kwa udhahiri basi kitatafutwa ama kuzushwa kitu,mtu ama jambo la kutupiwa mzigo wa lawama na kuundwa hoja nyingi za kurasimisha lawama hizo.

Ndivyo ilivyo kwa taifa letu la Tanzania pia,wakati ikiwa imesalia miaka minne tu ufike ule wakati ambao muda walioutumia wakoloni kututawala utalingana na muda tuliojitawala wenyewe kwa kuanzia na uhuru wa Tanganyika.Ni dhahiri tunazidi kupoteza haki ya kulaumu wakoloni kuwa ni wao pekee ndio waliotukwamisha kujipatia maendeleo màana haki ya kujitawala tulikwisha ipata na ikasalia wajibu tu wa kuilinda na kutetea haki hiyo.

Sasa muda wa kuwanyooshea vidole wakoloni unayoyoma na mataifa lukuki yaliyotawaliwa kama sie yamepiga hatua kubwa mengine yakiyapiku mataifa ya kikoloni yaliyowatawala ilhali sie tukisalia dhohofu kwa namna lukuki.Hayo yanazua mijadala mingi,mingi ikiwa na upeo na mingine ni ya kusaka visingizio tu mfano wa tumbili arukavyo tawi moja kulifuata lingine.Sasa baada ya kuona tawi la “laumu mkoloni” linadhoofika wengine  wameanza kutushauri turukie tawi la “laumu muungano na kutokuwepo Tanganyika”  

Tawi hilo linao wafuasi wengi tu kwasasa,nilishtushwa na kiongozi mmoja(sitamtja jina) wa chama cha siasa hapa kikubwa Tanzania alipotoa maoni yake katika mjadala mmoja kwenye mtandao wa Club House na kusema,”wazanzibari tayari wana chao na sisi tupewe Tanganyika yetu,kila mmoja afe na chake”.Si maneno mepesi hayo kwa kulingania na  hali na ukweli wa kihistoria wa mataifa mengi hapa Afrika.

Nani ni muumba wa Tanganyika

Wajerumani walipokuja hapa kusimika utawala wao “dhalimu” baada ya mataifa ya kibeberu kuona inawafaa kujigawia baina yao bara la Afrika mwaka 1884-5 huko Berlin walikumbana na ukinzani toka kwa wenyeji, mwanzo katika mtindo/sura ya kutetea himaya zao (mfano vita zilizoongozwa na Sultan Abushiri wa Pangani,Mtwa Mkwawa wa Uhehe,Mtemi Isike wa Unyanyembe,Mangi Meli na Mangi Sina wa Uchagga n.k), na baadaye kama sura/mtindo uliopevuka zaidi wa wafanyakazi/wazalishaji(mfano vita vya Majimaji).

Picha ya moja ya vikao vya mkutano wa Berlin.Kwa hisani ya mtandao

Wajerumani walilipatia jina eneo walilotwaa/jigawia kwa namna walivyoona inawapendeza wao mithili ya mtu atoavyo jina kwa mnyama wake anayemfuga ama kifaa chake cha kazi.Hivyo kuanzia Bagamoyo mpaka Ruhengeri(Rwanda) na Urundi, Udigo hadi Nyasa mpaka eneo la Kionga(leo lipo Msumbiji) eneo la kilomita za mraba 994,996 walipopatawala  wao wakapaita “Ujerumani ya Afrika Mashariki”(Deutsch-Ostafrika). 

Waingereza baadaye baada ya kuyarithi makoloni ya wajerumani(yaliyoporwa na wakubwa/mabeberu wenzie) wakalipa jina eneo hili ukiacha Rwanda na Burundi na kuliita “Tanganyika”, hivyo muumba wa Tanganyika kama mamlaka ya kidola(Territorial State) ni mkoloni wa kiingereza na si mzalendo mwenyeji wa kiafrika.

Wazee wetu waliodai uhuru wa Tanganyika ndicho walichokikuta,mapambano yalikuwa ni ya haki kwa mizani yote, ila kuuelewa muktadha ni vema kuweka wazi kuwa sababu iliyotoa msukumo wa kudai uhuru wa Tanganyika ilikuwa ni kuumizwa na “ushenzi” wa ukoloni ambao ulikwenda zaidi ya makabila,dini na jinsia zao hivyo wao pia hawakuwa na sababu ya kurudi kupambania kwa mpaka na ukomo wa Abushiri,Mkwawa na baadaye Kinjekiltile Ngwale.

Walijua kwa yakini kuwa daraja hujengwa ili kuvuka kuelekea mbele na wakoloni licha ya hila zao tayari walikuwa wameyaweka makundi mengi ambayo huwenda kabla yao(wakoloni) hayakuwa/hayakujuitizama kama mamoja.Hii haisemwi sana na wadai Tanganyika kuwa mara zote fikara yetu ilikuwa kupambana kupata/kwa kutizama “umoja mkubwa zaidi”(kutoka himaya za makabila baadaye wazalishaji ,kisha siasa za ukombozi kwa uzalendo wa kitaifa na kilele ni mapambano kusaka umoja wa Afrika katika msingi wa fikara za umajumui wa Afrika) wenye kuzizidi tofauti zenu ambazo nyingine zilipandikizwa na kukozwa na wenye kusudi ovu na zingine zilikuwako na watu waliishi nazo pasi magomvi.

Hadaa ya utanganyika na maendeleo.

Kwanini hali ya watanzania wengi ipo kama ilivyo sasa yaani dhalili,kijamii na kiuchumi? swali hilo linaibua  mijadala kila mahala na kila ngazi katika jamii yetu.Zipo hoja nyingi zinazotaja sababu kadha wa kadha kuljibu hilo.Kati ya hoja hizi hoja ya aina ya muundo wa kiutawala wa nchi yetu hasa muundo na aina ya muungano tulionao hutajwa kuwa ni changamoto na baadhi ya watu.Kwa wengine hoja hiyo ndio hoja kiini cha watanzania wengi kuwa katika hali dhalili,kanakwamba tukiwa na muundo tofauti wa utawala hasa muungano basi  ni tikiti ya sie kufaulu.

Wahanikiza hoja hiyo husema muundo wa sasa ndio chanzo cha manung’uniko,uonevu,kutokuwako demokrasi,utawala wa sheria na uwazi katika utawala hali inayopelekea umasikini na dhalilii,hivyo ukibadilika hayo yote yataondoka.Namna kubwa inayopendekezwa ya kuhuisha muundo huo ni kurejesha upya mamlaka ya Tanganyika kwa kuunda serikali ya Tanganyika na kuipa mamlaka kamili serikali ya Zanzibar (huwenda isiitwe tena serikali ya mapinduzi ya Zanzibar tena maana si wazanzibari wote huyakubadi mapinduzi yenyewe) kisha kusalia na serikali ya muungano ya kuisherehekea(ceremonial government).

Wadai Tanganyika huwasilisha hoja mbalimbali katika mnada wao lakini lengo ni “kutuhakikishia” kuwa ipo “pepo” tunayoikosa kwa kutokuwepo serikali ya Tanganyika hivyo tufanye hima tusije-endelea kukosa mambo mema(asali na maziwa) yatakayoletwa na uwepo wa Tanganyika.

Wadai Tanganyika wengi hunena kwa lugha sawa na ile yaliyotumia mataifa mengi kudai uhuru hapa Afrika yaani kulenga habari zihusuzo masuala ya utawala na nafasi zake.Mwanzoni kidole alinyooshewa mzungu leo ananyooshewa mswahili anayetenda sawa na mzungu yule,kisichosemwa kwa kina na wadai Tanganyika wengi ni kuwa mzungu yule na mswahili huyu “patano” lao li katika aina ya mfumo wa siasa-uchumi na si nyadhifa za utawala.

Ndio maana hata sasa mataifa takribani yote ya Afrika ambayo hayakuungana na Zanzibar kama ilivyo kwa Tanganyika hayatofautiani kihali yakiwamo yaliyobadilisha vyama na tawala(kwa fujo au kwa sanduku la kura) mara nyingi kushinda Tanzania.Mfumo huo wa siasa uchumi haubadilishwi kwa majina ya mataifa na kinadharia katika nadharia za siasa-uchumi unabadilika kwa wanaoumizwa na mfumo huo kufaulu kuungana na kuupindua mfumo huo kandamizi, kwa muktadha wa nchi yetu na kwa jicho la kitabaka  ni rahisi kuwaona wanaokandamizwa na mfumo huo kandamizi wa siasa-uchumi,

Hawa wanaokimbizwa mabarabarani na mashambani kila uchao ilhali watawala wakizuia waziwazi na kufifisha jitihada zao kujinusuru na unyonyaji na ukandamizwaji wao(kwa hila na mabavu) ilhali wasomi “wajanja” wakiidokeza miradi ya “kuwainua” madhalili wetu kwa mashirika makubwa makubwa yanayofadhiliwa kwa kiasi kikubwa na makampuni makubwa ya kimataifa yanayowanyonya madhalili haohao kwa namna tofautitofauti.

Chuki kwa muungano dhidi ya upenzi kwa Tanganyika.

Ni kweli Tanganyika kama mamlaka ya dola yenye mipaka iliuawa kwa hati ya muungano(kimantiki) na baadaye kwa mabadiliko ya katiba ya mwaka 1965(kisheria).

Muungano wa tarehe 26 April 1964 umekosolewa sana kuanzia nia yake ,namna ya uundwaje na utekelezaji wake kiasi ambacho lipo kundi la watu wengi lilioukatia tamaa.Na wengine hawazifichi tena,hofu,mashaka na chuki zao kwa muungano huo.Hofu,mashaka na chuki kwa muungano zinaweza kuhusianishwa ama kunasibishwa na upendo kwa Tanganyika yaani wengine wakadhani na kudhahanisha wengine kuwa kuutilia shaka ama kuuchukua muunguno na kuipenda Tanganyika ni jambo Mojave.

Nadhani si jambo moja kuuchukia muungano na kuipenda Tanganyika, na kwa muktadha wetu hata wenye kuijua Tanganyika si wengi na Tanganyika ilikuwa ni “tawala” si dhana ya kiimani mfano wa Mungu ama Shetani kwamba unawajibika tu kumpenda na kumtii ama kumchukia na kumlaani tu huku ukinyimwa haki ya kumfanyia uchambuzi wala kumkosoa , tawala inaweza kufanyiwa uchambuzi wa kiasayansi na ikaeleweka vema ,hivyo kuhusu Tanganyika tunaweza na tunapaswa kuulizana juu ya chanzo cha mapenzi yetu kwayo kwa kuzingatia kipindi cha miaka mitatu ya uhai wake.

Katika miaka yake mitatu ya uhai ilitupa yepi ya kukumbukwa kiasi cha kutamani irejeshwa kwa kuwa bila hayo iliyoyafanya basi hakuna mustakabali mwema wala hakuna namna ya kuyafanya nje wa uwepo wake(Tanganyika).Tusisahau kuwa masuala ya utawala(hasa suala la nyadhifa) licha ya umuhimu wake wote daima yamekuwa ni masuala yenye kuwahusisha wachache.

Sasa uzoefu wa kihistoria utufundishe tu kuwa inawezekana katika dai la Tanganyika haikusudiwi ukombozi wa wavuja jasho na mamlaka kwa wazalishaji walio wengi bali namna ya kufika juu kwa walioikosa njia katika mkondo mkuu. Kama sivyo tungekwishaziona dalili za wanadi utanganyika katika mavuguvugu yao na taasisi wanazozoziratibu wanajifungamanisha na agenda na mapambano ya ukombozi wa watu vinginevyo lugha na matendo yao yanawaweka pahala pengine

Nani wanufaika na mnada wa U-tanganyika

Kwakuwa hakuna dalili wala ishara zenye ithibati zinazoonesha kuwa uwepo wa serikali ya Tanganyika utakuwa ni muarobaini wa matatizo ya watu.Tunaweza kujifunza hili kwa namna mbili ,mosi kwa kupitia mifano ya wenzetu hapa barani Afrika ambao nao dola za mataifa yao na mipaka yake waliundiwa na wakoloni kama sie na labda wenzetu walikuwa na maarifa mengi hivyo hawakuingia katika “balaa” la kuungana na Zanzibar.

Je, wana mataifa gani ambayo tunapaswa sie kuwaonea gere ama kujilaumu na kuona tumepoteza sana na kupoteza kwetu ni kwasababu ya kuiua serikali ya Tanganyika.Hoja hapa si kufanya ulinganifu na waliofeli bali ni kuonesha kuwa inahitajika zaidi ya majina na idadi ya serikali kuufikia ukombozi wa watu waliofanywa dhalili kiasi yaa kuibua hisia na ufahamu wa kupambana kuusaka uhuru.

Pili tunaweza kuitizama miaka 3 ya uwepo wa Tangayika na kuifanyia uchambuzi wa kimuktadha wa kisayansi kwa skeli kubwa.Tukijielekeza katika hali na uelekeo wa watu kiustawi.Ukweli wa jumla ni kuwa tayari kulikuwako manung’uniko (bila kujali ya msingi au la),zipo rejea kadha wa kadha za wananchi wakimlamu kiongozi wa serikali wakati huo kuwa ameshindwa kujitofautisha na wakoloni.Mfano maarufu ni barua ya mwanakikiji mmoja wa kutoka huko Pawaga,Iringa aliyemwandikia barua ndugu Nyerere akimuhoji kwa kumlaumu kuwa je,ikiwa wakoloni wangetoza gharama kubwa katika elimu,baba yake Nyerere angemudu kumsomesha?.

Kulikuwako hali ya kupanda kwa gharama za maisha na huduma za kijamii kama elimu,afya n.k kuwa aghali na kugeuzwa bidhaa lakini manung’uniko makubwa yakiwa ni kuzaliwa kwa tabaka la warasimu ambao walijinufaisha wao kwa kutumia nyadhifa zao za uongozi na kulimbikiza mali (wabenzi) huku  wananchi wa kawaida “makabwela” wakiachwa solemba na kulaumiwa kuwa ni uzembe wao kutokuwa na visomo na kushindwa kwa msemo wa kileo “kuzikatama fursa”.

Kwa rejea hizo mbili basi ni haki kusema “msukule” huo wa Tanganyika hauna manufaa kwa wengi hasa wavuja jasho walio wengi kwakuwa  msukule huo haupo katika nadharia ama falsafa yeyote ya uchumi iliyowahi kuwepo ama kubashiriwa inayodhihirisha kwa ithibati kuwa itawakomboa na kuwaweka katika ustawi watanzania leo , ni jina la dola tu, dola tulilolirithi kwa wakoloni ambalo hatukufaulu kuliondolea sifa za dola za kikoloni na hiyo haimaanishi kulirejesha kutaziondoa sifa hizo.

Ni sawa na kusema leo tujipe jina jingine la “Jamhuri ya Majuha” ,ukweli ni kuwa hatutastawi ama kudumaa kwasababu ya jina hilo(labda kama tutageukia ushirikina wa kutenda kwa kuzingatia baraka na/ama laana) isipokuwa tutastawi ama kudumaa kulingania tunachokipanga ,namna tukipangavyo na hamasa yetu katika kulitekeleza.

Kikao cha Bunge.Mkutano wa Bunge la katiba.Picha kwa hisani ya mtandao

Wanufaika wa hiyo serikali ya Tanganyika itakuwa ni hao hao warasimu wa kiutawala kama ilivyo sasa,hao ndio wana hakika ya kunufaika na njia zao hazitakuwa tofauti na sasa za kuparurana,kufitiniana,kujipendeza n.k,wengine ambao si hamasa yao kugombania nafasi za utawala(kusaka heshima/kutambuliwa ama kulimbiza) hakitajwi nini watakipata na Wazanzibar wamewazuiaje kukipata leo,zaidi ni ahadi za hadaa kama tuzionazo katika majukwaa ya kutafuta kura.

Kinachofanywa nara nyingi na wadai Tanganyika ni kutengezeza dhana(kuiba/kuchezeaa hisia na fikra) kuwa huko nyuma kulikuwako na kitu chetu chema na bora sana ambacho tuliporwa na “mwovu” Nyerere,jambo ambalo hakuna ushahidi wowote wa kihistoria wa wema na ubora wa Tanganyika hiyo.

CCM wana kesi ya kujibu?

CCM mwana wa TANU na ASP ndicho chama kilicho katikati ya jambo hili la muungano.Hata madai ya kurejeshwa kwa serikali ya Tanganyika  yalianzia humo na kwa kweli yana nguvu zaidi humo ilikuwa hivyo zama za G55 ikawa hivyo katika bunge maalumu la katiba 2014.

Sasa kuhusu hili la “msukule” wa Tanganyika, CCM ambacho ndicho kiliiua hiyo CCM kuna kazi ya kufanya ambayo hakikuifanya na leo watu wanabeba mabeleshi kuifufua maiti hiyo ya miaka angalau 56.Kazi ambayo CCM hakikuifanya kwa ustadi  ni, kuhakikisha “ustawi wa watu na maendeleo vinapatikana”.Wapiga mbiu ya utanganyika kwa muda wote watatafuta hoja lukuki lakini egemeo pekee la kuzisimamishia hoja zao huwa ni , maendeleo.

Ndo kusema, wapiga mbiu ya utanganyika (na wengine ni watu makini tu) wanajua kuwa “ukisingizia” hoja ya maendeleo basi mwerevu na mjinga wote wakitizama watashuhudia bayana kuwa hali ya maendeleo ni duni kwa watu wengi hivyo ni rahisi kwa “mjinga” kununua hoja ya wapiga mbiu ya utanganyika kuwa hatupati maendeleo kwa sababu hakuna serikali ya Tanganyika na tutayapata itakaporejeshwa.

Wapo wenye vifua hata vya kuongopa kuwa wazanzibari wanawanyonya kiuchumi watanganyika.Hivyo hiyo humaanisha kuongeza hasira na uchungu kwa “wajinga” kuwa si tu kuwa hatuendelei kwa sababu hakuna serikali ya Tanganyika bali hatuendelei kwasababu ya “Vi-Zanzibari”.

Isivyobahati kwa wana CCM wengi hoja zao zimebaki zilezile kuwa umuhimu wa muungano ni kwasababu tulikuwa na miingiliano ya jamii na kuoleana, ndizo hoja zinazowatoka kirahisi vinywani wanazi wa CCM na wakibishiwa basi wanaita kwa haraka askari polisi na uhamiaji “kuwashughulikia” wanaowabishia hoja zao duni.

Bado CCM haijaoni hatari ya mamilioni ya vijana wasio na ajira kuzidaka bila kuchunguza hoja hizo za uongo kuwa wananyonywa na wazanzibari na kuamini ikija serikali ya Tanganyika watapata ajira.

Bado CCM hawaoni hatari kwa makundi ya wazalishaji mfano wakulima wadogo,wafugaji,wavuvi na wachuuzi wanaonyonywa waziwazi na mabepari na pia serikali yao kuwa  watakapoletewa dokezo na wasaka fursa za utawala kuhusu Tanganyika “yao” wanaweza kuona ni heri kuitafuta ahueni huko.

Ni kama mfano wa mtu aliyeko Wawi,Pemba anavyoweza kudhahania kuwa ukatili wa vyombo vya dola upo Wawi tu hivyo kwake kusema “Polisi wa Tanganyika” wanatuonea ni tiba nafsini kwake ndivyo hivyo mtu kutoka Ngorongoro anaweza kusema kwanini mi siruhusiwi kumiliki ardhi Zanzibar wao wanamiliki yetu na atasema hayo akiwa pembezoni mwa uzio wa eneo la takribani laki moja ambalo linamilikiwa na mtu asiye mzanzibari wala mtanzania.

Hatari hizo ni ngumu kuziona kwa wanaofikiri muungano ni kwaajili ya kuoleana(ndoa) maana hata kero kuu ya muungano ni moja tu nayo ni ,”hakuna ustawi wa kuridhisha watu”. Kero nyingine ni ziada ama visingizio.

Hivyo kwa kushindwa kuwaongoza watanzania kuupata ustawi wenye tija CCM inakaribisha vitimbi vya aina hii ,vinaanza kwa hisia za utaifa(utanganyika) ila kesho vitashuka kwa hisia nyingine ya ukanda,baadaye udini na kisha ukabila na hayo yote si mageni,hisia hizo (za kipumbavu) zipo hai kwenye jamii yetu.

Hivyo CCM inastahiki kabisa hukumu na kuchapwa kiboko na wavuja jasho wa nchi hii wa kutuweka rehani kwa namna na mtindo huo.

Wajibu wa wavuja jasho.

Ni rahisi mno kwa mtu aliye katika kibano kikali kuitafuta ahueni yeyote tu na kutojibidiisha sana kuzingatia madhara.

Wakati wa ukoloni wapingania uhuru waliwaambia wavuja jasho/makabwela kuwa ukombozi wao utaletwa TANU itakaposhika madaraka.TANU iliposhika madaraka viongozi wake wakakimbilia “kuzikaba” fursa walizokuwa nazo wazungu.

Lilipotangazwa  Azimio la Arusha(waraka wa kimapinduzi kuwahi kuzalishwa nchi hii),wavuja jasho/makabwela wakaahidiwa kuwa mustakabali wa nchi utakuwa chini ya wakulima na wafanyakazi, wakatumaini.Ila warasimu wakahakikisha mamlaka hayarudi kwa wakulima na wafanyakazi na yanahodhiwa na dola.

Tulipogeukia mageuzi ya uchumi wavuja jasho/makabwela wakaambiwa  wataupata uhuru wa biashara na uchumi lakini wakaishia kuporwa ardhi,kufukuzwa maeneo yenye rasilimali na walipogeukia uchuuzi(umachinga) wakaambulia mikong’oto, dola likageukia kufanya ukuwadi waziwazi na “kuwapiga kabali” wale wote wasioridhishwa na kukabiliana na uporaji wa rasilimali za nchi na za wavuja jasho.

Na leo tupo katika ngazi ambayo dola halijali ,kutii wala kusikiliza maoni,mawazo wala hisia za wavuja jasho.Hali ya kiburi imefikia upeo kiwango ambacho mwandamizi wa serikali(sehemu ya dola) anaweza kuwaambia hadharani wavuja jasho kuwa pendekezo ama uamuzi wa serikali ukishatoka basi wote mnapaswa kukaa kimya, hapana kuwa na maoni na mwenye maoni tofauti ahame nchi.Hii imeshuhudiwa hivi karibuni katika sakata la wavuja jasho kutwikwa mzigo mwingine wa kodi/tozo.

Hayo yote ni mafunzo ya kihistoria kwa wavuja jasho, kuwa toka zama za mkoloni dola limekuwa likiwachukulia wao kama mfugaji aionavyo mifugo yake.Hali hiyo haikubadilika hata baada ya kupata uhuru hata nyakati zinazotajwa kuwa tulipata watawala waungwana wenye kuheshimu wavuja jasho bado dola liliendelea kujivika sifa ya “unyapara” sawa na dola ya kiloloni.Wavuja jasho lazima waelewe hayo ili wasihadaiwe tena na siasa za madaraka zenye lengo tu la kushika dola hilihili la kikoloni.Kulipa jina ya Tanganyika ama Tanzania hakuliondolei sifa hizo,hivyo suluhu kwao si serikali ya Tanganyika.

Wavuja Jasho lazima wajue(na watekeleze kwa matendo) umuhimu na ulazima wa umoja na mshikamano wa kimaslahi unaoakisi tabaka lao.Ni hatari mara dufu kwa wavuja jasho kwa kutokuwepo na vyama vya ushirika vyenye tija na vyama vya wafanyakazi vyenye tija kushinda kutokuwepo na chama cha siasa hata kimoja.Vikundi/vyama/na mashirikiano ya wazalishaji na wafanyakazi ndilo egemeo pekee la kulitumaini tena linalolinda maskahi yanayoshikika kwa wavuja jasho 

Hivyo wakati wanaovizia nyadhifa/fursa za kiutawala wanaidai Tanganyika kwa kufa na kupona wavuja jasho wajifunge mikanda kuunda vyombo vyao imara mfano hivyo vyama vya wafanyakazi na vyama vya ushirika na wauvunje mpaka wa “kijinga” unaojengwa na “vyama vya siasa”,makundi ya kidini na ya kikabila ambayo yanawatumia wavuja jasho kuhakikisha maslahi ya watu wengine huku wakihadaa kuwa ni mapambano ya haki kwa wavuja jasho.

Wavuja jasho hawatavuna lolote la maana kwa kuabudu “sanamu la Tanganyika”.Maana jitihada za kuuenzi msukule huo zina muelekeo wa kisiasa wa tabaka moja katika jamii kugombana baina yao katika jitihada kuuenzi mfumo uleule wa siasa-uchumi wa kinyonyaji Kwa kutumia dola lenye sifa na hadhi zote za la kikoloni

Muhemsi Mwakihwelo ni mwananchi wa nchi ya Tanzania.

Tumeyanakili makala yake haya katika ukurasa wake wa facebook

barua pepe yake ni;

muhemsimwakihwelo@gmail.com

Leave a Reply

Fill in your details below or click an icon to log in:

WordPress.com Logo

You are commenting using your WordPress.com account. Log Out /  Change )

Twitter picture

You are commenting using your Twitter account. Log Out /  Change )

Facebook photo

You are commenting using your Facebook account. Log Out /  Change )

Connecting to %s

SAUTI YA UJAMAA

Welcome to the Socialist Voice

Discover WordPress

A daily selection of the best content published on WordPress, collected for you by humans who love to read.

The Daily Post

The Art and Craft of Blogging

WordPress.com News

The latest news on WordPress.com and the WordPress community.

%d bloggers like this: