Na Gikaro B. Makera
“Enyi wavujajasho wote unganeni. Hamna cha kupoteza ispokuwa minyororo ya utumwa mliofungwa”.
Hali ya Muundo wa kitabaka Kabla na Baada ya Ukoloni
Katika nyakati hizi za ubepari wa Kilibelali mamboleo upo mpasuko mkubwa wa kitabaka katika jamii yetu, pengine tofauti na siku za miaka ya 1950 kuja 60 barani Afrika ambapo akina Senghor, Nkrumah, Nyerere n.k, walioona Afrika ni mahali palipokuwa hapana mgawanyiko wa-kitabaka. Kwa hoja kwamba kulikuwa hakuna Waafrika wachache waliokuwa wamehodhi njia kuu za maendeleo na kuweza kuwanyonya Waafrika wenzao wasio na uhodhi huo ila waliofanya hivyo walikuwa wakoloni kutoka huko ulaya.
Kwa maana hiyo ni kwamba hapakuhitajika mapambano ya kitabaka kufikia jamii ya kijamaa. Ingawa kiukweli ulikuwa ni uongo uliolenga kufumba baadala ya kuangaza kwa maslahi tabaka tawala. Ni uongo kwasababu kwa kiasi kikubwa mahusiano ya kikoloni yalibakia kama yalivyo. Ni mahusiano yaliojikita katika unyonyaji na uporaji wa jasho la wavujajasho waliokuwa Afrika kwa usimamizi wa mameneja weusi na haya yote matokeo ya kwamba ubepari ndio ulikuwa mfumo wa maisha ulimwenguni (capitalist international social system) kama bado ilivyo sasa na hivo uhusiano au msigano ulibaki kuwa mabepari wa ulimwenguni na wavujajasho ulimwenguni na ambapo Afrika na Tanzania zipo. Hili litafafanuliwa kwa huko katika aya zifuatazo za Makala haya.
Sasa kufahamu mchakato na chimbuko na mundo wa-kitabaka Tanzania na Afrika (nitazungumzia hapa Tanzania,ingawa spendi kuacha kuitaja Afrika kwa maana kinachochukua nafasi Tanzania katika masuala nyeti ya “Siasa-Uchumi hakina tofauti na huko Kenya,Uganda, DRC-Congo na kadhalika) yabidi kuchunguza kihistoria na kimahusiano. Matabaka yalishaanza kuwepo Afrika hata kabla ya ukoloni, ukoloni ulichofanya ni kuyaimarisha kwa manufaa yake na hatimaye pia ulibua matabaka yenye sura ya Kibepari. Ukoloni uliimarisha matabaka kwa manufaa ya kutawala kwa mantiki ya yakutenga na kutawala (Divide and rule). Sisemi tu kuwa matabaka yanakua kwa kuwagawa watu sanjari na hilo huibuka kutoka katika mchakato mzima wa uzalishaji mali unaoegemea katika misingi ya unyonyaji na uhodhi binafasi.
Ni kweli baadhi ya sehemu kwa mfano Tanzania kulikuwa hakuna mgongano wa kitabaka mkubwa kama ilivyokuwa huko Ulaya Katika karne hiyo ya 19, kulikuwa na baadhi ya sehemu zilizo na mgongano huo kama huko Kagera ambako kulikuwa na falme ya kikabaila ya Karagwe ambapo ardhi kama msingi mkuu wa wa mfumo wa Ukabaila ilikuwa ikimilikiwa na wachache; Hasa waliokuwa na uhusiano wa karibu na himaya hiyo ya Karagwe jambo lililosababisha kuzaliwa kwa tabaka la Manokoa (Watwana) wakiwa hawana ardhi badala yake walitumia ardhi ya kabaila kwa masharti ya fidia ya kufanya kazi kwa siku kadhaa kwenye shamba la Kabaila au kumlipa mazao baada ya kuvuna.Hali kama hiyo katika zama zetu hizi karne ya 21 nimeiona katika sehemu za huko Tanga ambapo watu hukodishwa shamba na kutakiwa kulipa kwa mazao.
Vile vile kulikuwa na jamii nyigine kama hizo hapa Tanzania zilikuwa katika hatua ya Ukabaila wa wastani (semi-feudal) kama vile wagogo, wanyamwezi, wahehe n.k. ambapo kiongozi alichaguliwa kulingana na kigezo cha umiliki wa mali. Lengo langu hapa ni kusisitiza kuwa ukoloni uliuwa hatua hiyo muhimu ya ukuaji huo wa kitabaka wa ndani na Ukabaila wenyewe kama mfumo wa maendeleo ya binadamu na kuibua sura nyingine ya kitabaka yenye viashiria vya Kibepari. Liliibuliwa tabaka la wavujajasho (wafanyakazi wa mashambani, migodini, misituni, hifadhini/mbugani, viwandani na wazalishaji wadogo kwa sababu walikwepo wakubwa) kwa maana moja tu kwamba, hili tabaka halikuzalisha moja kwa moja kukidhi mahitaji yake bali mahitaji ya Wakoloni. Sambamba na hilo palikuwepo na tabaka la walanguzi kwa niaba ya wakoloni wa kibepari, tabaka ambalo lilishehenezwa na watu wengi wa Asia na mwisho ni wakoloni (Mabepari) wenyewe.Kwa muktadha kama huu tunaweza kusema palikuwepo na mgongano wa kitabaka kati ya Mabepari wa Kikoloni na washirika wake (walanguzi na mameneja) na wale wavujajasho.
Ndiyo katika hali hiyo kama ushaidi wa kihistoria na kimazingira unavyoeleza kutokana na “msuguano huo wa kitabaka kati ya wakoloni na wenyeji ulipelekea mapambano kadhaa ya kivita hasa hasa vile; vya maji maji (1905-07) ambapo inaripotiwa kuwa maelfu ya wavujajasho walipoteza maisha na makazi kutokana na ukatili wakikoloni wa-kibepari uliotumia mbinu mbali mbali za kikatili kupambana na mavuguvugu ya wavujajasho Watanzania. Wakoloni walichoma makazi,mazao na kulipua mabomu kwenye maeneo ya wenyeji wavujajasho walioupinga ubabe wakikolon.
Baada ya kusema ukoloni umekwisha bado mpasuko wa kijamii uliendelea kubakia kama ulivyo na hii inatokana na ukweli kwamba wale maintelengentsia yaani watu waliokuwa wamesomeshwa na kupata elimu ya kikoloni kwa lengo la kusaidia shughuli za utawala na uporaji ndio baadhi yao waliamua kupora mapambano halisi ya wavujajasho kutoka kwenye ajenda kuu ya kutatua mgongano wa kitabaka na mahusiano ya kinyonyaji na kuyahamishia katika ajenda ya Utaifa mwepesi (parochial nationalism) kwa sura yaKijenetikali (rangi) baadala ya historia yenyewe iliyowafanya kuwa katika hali ya udhoofu na ufakara. Tizama zaidi chapisho la muundo wa dola na ujenzi wa kitabaka Tanzania na ndugu Walter Rodney (state formation and class formation in Tanzania, 1973; Maji Maji).…. (Itaendelea)