Siku Ya Ukombozi wa Bara la Afrika 2020: Mwendelezo wa Mateso Yasiyokoma

Na Muhemsi Mwakihwelo

“Hata hivyo ewe mtoto mweusi/wa kiafrika, katika unadhifu ama Dhalili umezaliwa katika haya na katika udhaifu ama dhalili utakufa kwayo”

Steve Bantu Biko

Sehemu ya II

(Sehemu ya kwanza ya makala hii inapatikana hapa)

Kawaida, raia wa mataifa makubwa makubwa afanyapo makosa ughaibuni mataifa hayo humkingia kifua raia wao na wakati mwingine huviwekea vikwazo “vi nchi” vidogo vyenye kuwatia mbaroni raia wao. Hali ni kinyume kabisa kwa mataifa ya Afrika na hata pia  Umoja wa Afrika. Wao hawawezi kuwakingia kifua wananchi wao wala kuwatetea. Yakikukuta huko ughaibuni basi jipiganie mwenyewe na ukweli ni kuwa hata takwimu za watu wetu waliopo huko ni za mashaka matupu. Hawa wanaovuka jangwa la Sahara na kisha bahari ya Mediterranea tulichoweza kusema sisi ni “wamejitakia wao wenyewe”.

Hivyo, haitegemewi sana kwa nchi za Afrika na Umoja wa Afrika kuzungumza ama kukemea juu ya ubaguzi na mauaji ya watu weusi wa Marekani na Ulaya  kwa namna thabiti; maana kufanya hivyo kuna leta “hatari” ya kuwaudhi “wakubwa”, jambo ambalo hatuna mataifa yenye utayari huo kwa hofu ya kuhatarisha tonge la misaada na zaidi vikwazo.

Haitokei mara nyingi waafrika kubishana juu ya umuhimu wa muungano wa mataifa ya Afrika. Kinacho bishaniwa mara nyingi ni namna ya kulifikia hilo na mikingamo iliyopo. Kwa maoni yangu kazi kubwa ni “ususi wa mbadala  dhidi ya kilichotufanya dhalili kwa pamoja”.

Katika hili napendekeza ulazima wa kutizama mifumo ya uzalishaji mali na tamaduni zake zilizoikwida Afrika kwa pamoja na kuzitafutia mbadala wa mifumo ya uzalishaji mali na tamaduni zenye kututoa katika ushawishi wa mifumo ile ile iliyotufanya dhalili na inaendelea kutufanya hivyo.

Kwa hoja dhahiri ni kuwa tulifanywa dhalili na mifumo ya uzalishaji mali na tamaduni zake, yaani ubepari na tamaduni za “uzungu kuu”(white supremacy), ukaburu (ubaguzi wa rangi) n.k. Hivyo mbadala tunaopaswa kuuelekea sharti uweze kukabiliana na hayo na zaidi uweze kukabiliana hata na mifumo ya uzalishaji na tamaduni kandamizi zilizokwisha kuwapo kabla ya wakoloni mabepari kututawala. Hii ikijumuisha ukabaila na tamaduni kama unyonyaji wa kijinsia, ushirikina(mauaji ya albino, vikongwe, walemavu ), ukeketaji n.k. Kwani, licha ya kuwa mambo hayo yalikuwapo hapa kwetu kabla ya ubepari kuja, hayatusaidii na yanafifisha jitihada na kasi yetu katika kujipatia ustawi na hasa kujihami dhidi ya jamii zenye nguvu zilizopiga hatua ya kimaendeleo leo.

Ni wajibu wa kizazi cha leo kuanza kuchukua hatua za kuwanusuru waafrika, kuwaunganisha na kujenga jamii yenye nguvu. Fikra na matendo ya kimapinduzi ndo “njia iliyosalia na ni moja”. Sasa waneni hunena ya kuwa “Isiyokuwasha, Hujailamba”, ndo kusema licha ya kuwa kuna kundi liitwalo waafrika, ila si wote wameathiriwa kwa namna sawa, wengine wamechagua ukibaraka, wengine uwakala lau wengine kwa kudra (ikiwa twaamini juu ya kudra) wanarandana kwa tabaka hata na tunaowaita wanyonyaji. Hivyo hawataona haja ya kufanya lolote la kimapinduzi kugeuza hali iliyopo maana hawana maumivu wayajuayo. Hivyo, walio dhalili na duni miongoni mwa waafrika kuanzia Marekani, Ulaya, Karibeani na Afrika kwenyewe ndio haswa jukumu hilo lapaswa kuwa lao.

Ni muhimu kutambua a michango ya fikra mbalimbali zilizoibuliwa na waafrika na kutumiwa kama silaha dhidi ya fikra na nadharia zilizopelekea kukwamisha mchakato wa ustawi wa waafrika na uhuru wao. Fikra hizo ni pamoja na Umajumui wa Afrika, Afrisentrisiti, Ujamaa, Urastafari, Nuwaubiani, Vodoo, Kwanzaa, na hata baadhi ya makundi katika zifahamikazo kama Dini kubwa walijaribu kufanya uasi dhidi ukandamizaji wa waafrika, baadhi yao ni Askofu Kimbangu huko Kongo DC, Paul Bugle huko Jamaika, Askofu Chilembwe huko Malawi, Mchungaji Martin Luther King Marekani, Sadaurna Dan Fodio huko Sokoto, Al Mahd huko Sudan, Kinjekitile Ngwale kwa iliyokuwa Tanganyika, Elijah Mohamed na Malcom X huko Marekani.

Kila moja wapo ilichangia kupunguza makali ya ukandamizaji na kutoa tumaini la ukombozi kwa waafrika waliokuwapo madhilani, ingawa suluhu ya kudumu haikupatikana. Kizazi cha leo licha ya kuyafahamu hayo yote kinawezaje kukumbatia fikra na mifumo iliyowasababishia madhila na kumtegemea mwisho mwema?

Kama ambavyo madhara ya wazi ya ukoloni mkongwe ilikuwa ni kuigeuza Afrika soko la kila kinachoundwa katika viwanda huko Ulaya na Marekani, sasa kwa sheria za kimataifa (sheria ya wenye nguvu), hasa kupitia uratibu wa shirika la biashara la ulimwengu (WTO), viwanda vyaweza kuwepo hapa hapa na vinalindwa kwa umakini na dola zetu na kupitia sheria za uwekezaji wa kimataifa (FDI). Ndivyo hivyo, hata katika nyakati hizi sasa za ukoloni mamboleo sisi ni soko kuu “Supemarket” tu ya vyote kuanzia silaha, dawa, mitambo mikubwa na midogo, mavazi (ambayo yamekwisha valiwa na wengine), vifaa vya kielektroniki (simu, radio, saa), mazao ya kilimo (vyakula, bidhaa ngozi) na takribani kila kiundwacho na watu/ binadamu chini ya jua.

Janga la ugonjwa wa mlipuko wa Corona, almashuhuri Covid-19, limeendelea kutusisitiza sisi kuwa tunapaswa kujimudu la sivyo itakuwa rahisi kwetu kuangamia au kuangamizwa (ikiwa yupo mwenye/ chenye nia ya kutufanyia hivyo).

Kwanini mpaka leo tunakubali kuwa soko la dawa na kila tujadilipo bajeti zetu tunaona ni suluhu kwetu kuongeza bajeti ya ununuzi wa dawa na vifaa tiba bila kuzingatia kuwa tunapalilia uraibu wa uteja kwa makampuni hodhi ya biashara ya dawa (Pharmaceutical Multinational Companies)? Kuzidisha bajeti ya ununuzi wa dawa ni jambo la suluhu ya masafa mafupi na tafsiri yake ni kuwa tunataka watu waugue ili wanunue dawa. Hiyo ndio kiu ya makampuni makubwa ya dawa, ili yazidishe kupata faida. Kwanini tunakubali uteja/ uraibu huo?

Kwanini tusiongozwe na falsafa ya “kudhibiti watu wasiugue ili tusilazimike ama tupunguze mzigo wa kununua dawa na vifaa tiba hasa mitambo ya kisasa ambayo hatuna uwezo wa kuiunda hapa”? Wakyuba wanafanikiwa mno kwa kuwa falsafa hiyo ndio inaujenga mfumo wa afya katika kisiwa kile.

Unawekeza katika utafiti, hasa wa Chanjo na Dawa za Magonjwa, unazalisha wataalamu wa afya kwa uwiano wa idadi ya watu wako, unawaheshimu na kulinda maslahi yao. Badala ya kuwa na balozi wa nyumba kumi, ambaye kazi yake ni kusifia maamuzi ya watawala, unakuwa na daktari wa nyumba ishirini (20) sambamba na muuguzi na wataalamu wengine wa afya, wenye uwezo hata wa kuwafikia watu katika nyumba zao na kujua mtindo wao wa maisha, ikiwemo chakula walacho, usafi wa maji, historia ya afya ya familia, hali ya usafi wa miili na mazingira yao.

Tafiti lukuki zimekwishaonesha kuwa magonjwa mengi sumbufu yakiwemo ya milipuko, mathalani kipindupindu, homa za matumbo na hata magonjwa yasiyoambukiza, mfano shinikizo la damu na kisukari, hutokana na mtindo wa maisha. Hivyo, stadi na kanuni za afya, mfano usafi wa mwili, kunywa maji safi, mlo kamili, mazoezi vinaweza kupunguza mno hatari ya watu kupata magonjwa hayo na hivyo kupunguza mahitaji makubwa ya madawa na vifaa tiba, hasa ambavyo ni aghali na hatuwezi kuviunda hapa Afrika.

Sasa ikiwa tutapata watu wenye afya bora ipo hakika ya kuwa na wajenzi wa Afrika wenye utimamu na sio wajenzi duni. Fikiri, laiti tungekuwa na daktari wa nyumba kumi kila kijiji na kila mtaa, kama tulivyokuwa na Shekhe, Mchungaji na Muaguzi takribani kila kijiji na mtaa, huwenda kila baada ya nyumba tano, Malaria na Kipindupindu vingekuwa na hali gani?

Je, nasi kama Bara, tungewekeza katika utafiti wa dawa na chanjo, toka Ghana ilipopata Uhuru wake 1957, tusingekuwa na dawa yetu kama ya Alpha B ya Wakyuba ama zaidi?

Wakati wataalamu wa Taasisi ya John Hopkins wakiwa Milima ya Karatu kusaka utaalamu wa Wahadzabe, tunaowaona kuwa ni watu na jamii duni, sisi tunajigamba kuongeza bajeti ya ununuzi wa dawa. Dawa ambazo huwenda maarifa yake yamechumwa hapa, kisha zikazalishwa katika viwanda kwao na kisha zikasajili na kujimilikisha haki zote juu ya dawa hizo (Intellectual na Property Rights); ambapo maana yake hata sisi hatutakiwa kuzitengeneza dawa hizo bila ridhaa yao. Hiyo ndio njia tulioichagua waafrika miaka 62 baada ya kutangaza habari ya “Siku ya Ukombozi wa Bara La Afrika”.

COVID-19 imetutingisha na Umoja wa Afrika umeonekana mianya yake yote maana sasa tumejikita kufungiana mipaka tu, Wakenya kuwafungia Watanzania na Wasomali, Watanzania kuwafungia Wakenya, Wazambia kuwafungia Watanzania hiyo ndo habari isikikayo. Ila mataifa yote mwanzo yalipoambiwa kuzifungia mipaka hasa ya viwanja vya ndege nchi zilizoathiriwa zaidi na Covid-19, takriban zetu zote “ziliufyata” kwa hofu ya kutowaudhi mabwana wakubwa wa dunia na pia kulinda mapato (faida dhidi ya Utu) na zingine hazikitangaza kuzuia mashirika ya ndege Kuja nchini kwao mpaka yalipoamua yenyewe kuacha.

Sote twajua kwa hakika kuwa hali ya bara la Afrika na waafrika wenyewe  si njema sana hivyo tusithubutu kujiongopea kuwa lipo chaka ambala tutajificha huko kisha turudi tukiwa tumeendelea. Ikiwa tutaendelea basi tutapaswa kuendelea huku ulimwengu ukitushuhudia na njia ya kutufikisha huko ni “MAPINDUZI”. Ni kupitia mapinduzi ndipo mirija ya unyonyaji itakatwa na madhila yatakoma.

Afrika Moja! Afrika Huru! Afrika ya Kijamaa!

Leave a Reply

Fill in your details below or click an icon to log in:

WordPress.com Logo

You are commenting using your WordPress.com account. Log Out /  Change )

Twitter picture

You are commenting using your Twitter account. Log Out /  Change )

Facebook photo

You are commenting using your Facebook account. Log Out /  Change )

Connecting to %s

SAUTI YA UJAMAA

Welcome to the Socialist Voice

Discover WordPress

A daily selection of the best content published on WordPress, collected for you by humans who love to read.

The Daily Post

The Art and Craft of Blogging

WordPress.com News

The latest news on WordPress.com and the WordPress community.

%d bloggers like this: