AZIMIO LA MANZESE (THE MANZESE RESOLUTION)

AZIMIO LA MANZESE

JUU YA KUBOMOA MIFUMO YA KINYONYAJI YA UKOPESHAJI FEDHA NA KUJENGA MIFUMO MBADALA INAYOENDESHWA NA KUMILIKIWA NA WANYONGE

Sisi wanawake, wengi wetu tukiwa ni wanyonge tunaojishughulisha na biashara ndogo ndogo katika jiji la Dar es Salaam, tumekutana leo tarehe 9 Marchi 2019 katika eneo la Manzese kwa ajili ya kuadhimisha Siku ya Wanawake Duniani. Tuliohudhuria Kongamano hili hatukuwa wanawake peke yetu, walikuwepo pia wanaume, wengi wao wakiwa vijana, walioungana nasi kwa ajili kubadilishana uzoefu juu ya dhahma tunazokumbana nazo ndani ya mfumo wa kinyonyaji wa soko huria na namna ya kukabiliana nazo. Baada ya majadiliano ya muda mrefu, tumeazimia yafuatayo:

(1) Tunahitaji majukwaa mbadala ya wavujajasho

Sisi wanawake wanyonge tumekuwa tukitumiwa sana na watu wa tabaka la juu (wanaume kwa wanawake) kupamba mikutano yao, iwe ni ya vyama vya siasa, taasisi zisizo za kiserikali au taasisi za kibiashara. Tutavalishwa fulana na vitenge, na kupewa soda na vyakula katika mikutano hiyo, lakini ukweli utabaki kuwa mikutano hiyo sio ya kwetu. Tunatumika kama vikaragosi tu ili kutimiza maslahi ya watu wa tabaka la juu ya kutafuta fedha na madaraka. Kongamano letu la wanawake wavujajasho limetufunza kuwa sisi wanyonge tunahitaji majukwaa mbadala, yaliyo mikononi mwetu wenyewe, ambapo tutakutana ili kubadilishana uzoefu na kuweka mikakati ya kupambana na mifumo inayotutesa na kutukandamiza. Hakuna mtu wa tabaka la juu atakayetukomboa: sisi wanyonge tutajikomboa wenyewe, na silaha yetu kuu ni umoja na mshikamano miongoni mwetu.

(2) Tunanyonywa, tunateswa na kudhalilishwa na taasisi za mikopo

Sisi wanawake wanyonge wa mijini tunaojishughulisha na biashara ndogo ndogo tumejikuta tukilazimika kuchukua mikopo kutoka katika taasisi za mikopo midogo (microfinace) na benki ambazo zimekuwa zikijinadi kuwa zimelenga kumkomboa mnyonge. Lakini ukweli ni kwamba taasisi hizi zimelenga kutuangamiza kabisa kwa kutunyang’anya hata kile kidogo tulicho nacho. Riba inayotozwa na taasisi hizi ni kubwa sana, mara nyingi huanzia asilimia 50 na kwenda hadi asilimia 200, ndani ya muda mfupi. Juu ya riba kuna makato makubwa, yakiwemo malipo ya kuombea mkopo, na masharti magumu ambayo hayatekelezeki. Taasisi hizo humtaka mnyonge aliyechukua mkopo aanze kuurejesha ndani ya muda mfupi, ikiwezekana ndani ya siku mbili. Je, mama aliyechukua mkopo huo atakuwa amefanya biashara yake kwa muda gani hata aanze kurejesha mkopo huo ndani ya muda mfupi?

Kutokana na riba za juu na masharti yasiyotekelezeka, faida kidogo tunayoipata kutokana na shughuli zetu inaishia kwenda katika taasisi za mikopo. Mara nyingi tunalazimika kuchukua mkopo kutoka taasisi moja ili kulipa mkopo katika taasisi nyingine. Tumejikuta katika lindi lisiloisha la unyonyaji kwa njia ya mikopo.

Taasisi hizi za mikopo zimekuwa zikishirikiana na vyombo vya dola kutunyanyasa, kutudhalilisha na kupora kila tulicho nacho, vikwemo vitu vya ndani. Wengi wetu tumejikuta tukiingia katika migogoro ya kifamilia hata kupelekea kuvunjika kwa familia baada ya kufilisiwa na taasisi za mikopo. Tunajukuta katika mifarakano ya kijamii na hata kujengeka uadui miongoni mwetu kwa sababu kampuni za mikopo zinatutumia sisi wenyewe kupitia vikundi ili tudhalilishane na kufilisiana. Wapo wengi wanaougua magonjwa mbali mbali, hasa magonjwa ya moyo, kudhoofika kiafya na hata kufikia uamuzi wa kuondoa uhai kutokana na udhalilishaji na unyang’anyi unaofanywa na taasisi za mikopo. Hatuwezi kukubali hali hii iendelee.

(3) Sasa basi: tuungane ili tujiondoe katika mfumo kinyonyaji wa mikopo

Tunaazimia leo hii kuwa ni lazima tujiondoe kutoka katika mfumo wa kinyonyaji wa mikopo. Tayari tunao uzoefu wa kuendesha vikundi vya akiba na mikopo ambavyo tumevianzisha sisi wenyewe na tunaviendesha kwa uwazi na demokrasia, na faida tunayoitengeneza inarudi mikononi mwetu sisi wenyewe. Ni wakati sasa wa kuunganisha vikundi hivi ili tuunde benki yetu wenyewe na pia tushirikiane kuanzisha katika miradi ya uzalishaji kwa njia ya ushirika kwa ajili ya maufaa yetu wenyewe.

Kwa hiyo, tumeamua kuwa, baada ya kuhitimisha Kongamano la leo, tutachukua hatua zifuatazo:-

(a) Viongozi wa vikundi vilivyo chini ya taasisi za mikopo wakutane ili wapange mkakati wa kujiondoa kwenye taasisi hizo, na kuvibadili vikundi hivyo kuwa vikundi vya akiba na mikopo vilivyo chini ya wanyonge wenyewe.

(b) Viongozi wa vikundi vya akiba na mikopo vilivyo chini ya wanyonge wenyewe wakutane kwa ajili ya kupanga mikakati ya utekelezaji wa azimio la kushirikiana katika kuanzisha taasisi za ushirika wa akiba na mikopo, pamoja na ushirika wa uzalishaji.

(c) Sisi sote tuliohudhuria Kongamano la Wanawake Wavujajasho turudi katika jamii zetu na “kueneza fitna” dhidi ya kampuni za mikopo. Tusikubali kuwaona akina mama na wanyonge wenzetu wakiendelea kurubuniwa ili wazifaidishe kampuni binafsi za mikopo. Tutumie kila mbinu kuhakikisha kuwa kampuni hizi zinatokomea kabisa.

(d) Zaidi ya hapo, tuwahamasishe wanyonge wenzetu nchi nzima wajiunge katika vikundi vya akiba na mikopo, na kisha waanzishe mashirikiano baina ya vikundi hivyo ili kujenga taasisi mbadala za mikopo na uzalishaji zilizo mikononi mwao wenyewe, zinazoendeshwa kwa uwazi, demokrasia na usawa, na zinazorejesha faida kwa wao wenyewe.

(e) Tunawasihi vijana wasomi, wanahabari, wanasheria, walimu, wahasibu, waandishi wa habari na wengineo kutumia ujuzi wao katika kutuunga mkono katika utekelezaji wa mambo yote tuliyoyaazimia.

Hii ni vita: vita dhidi ya unyonyaji, ukandamizaji na unyang’anyi unaofanywa na kampuni za mikopo. Sisi wanawake wanyonge tutaongoza mapambano ya kupigana vita hii mpaka pale ushindi utakapopatikana.

Zitokomee Kampuni za Kinyonyaji za Mikopo

Ukimgusa Mwanamke, Umegusa Jabali

Hakuna Usawa wa Kijinsia Nje ya Usawa wa Kitabaka.

Azimio Manzese 2

Advertisements
Categories:

4 Comments

 1. Ni ukweli usiopingika kwamba faida apatayo anayejitegemea ni kubwa zaidi ya ile apatayo aliye tegemezi kimtaji.

  Hata hivyo utegemezi kimtaji uliyolenga kukuza na/au kupanua biashara iliyotokana na mtaji mdogo wa kujitegemea uliopo hukuza faida haraka haraka zaidi ya ule uwekezaji wa kujitegemea mtaji mdogo uliopo usiotaka kukuza na/au kupanua biashara kwa njia ya kuikopeshea kutoka kwa wengine.

  Hivyo¸ badala ya kukataa kukopa kwa wengine¸ endelezeni kukuza na/au kupanua biashara zenu zilizotokana na mitaji yenu midogo ya kujitegemea iliyopo kwa njia ya kuzikopeshea kutoka kwa wengine ili nanyi muweze kuwa matajiri wanaojikopesha wenyewe na kukopesha wengine mapema iwezekanavyo.

  Like

 2. Hakika wanawake mnanyanyaswa na kukandamizwa sana na hizi taasisi za mikopo, ambazo ngozi zao ni za kondoo ilhali ndani ni chui .. Kila la kheli katika mapambano na ukombozi wa nafsi zenu maana mikopo hiyo inahangaisha sana nafsi za nyie wanawake ..

  Like

 3. Andiko hili fupi liwe mwanzo wa mjadala wa namna sahihi ya kusaidia, kuwezesha, kushirikisha na kufanya kazi na wasichana na wanawake. Kampuni nyingi, si tu hizi za mikopo, zinanyonya wanawake na jamii ya watu wenye fursa finyu. Riba inayowekwa juu ya mikopo ni kubwa mno. Ni ngumu sana kurudisha mkopo na hivyo wanawake wengi huangukia kwenye kundi la wanaonyang’anywa mali zao sababu ya kushindwa kulipa mkopo. Na kwa bahati mbaya, shida huwafanya wanawake warudi hukohuko kwenye mikopo hata pale wanapojua hatari zinazoambatana na mikopo hiyo.

  Like

 4. Nimesoma nivyoelewa mimi:Hili andiko halitaweza kuimarika ndani ya mfumo huu tulionao sasa,Mpaka sasa Siasa zimeshatugawa in groups,upendeleo,kuangaliana,n.k..Ushauri wangu ni : wote tusimame kwa bidii kwanza tuweke mustakabali wa matengamano ya wananchi wawe na umoja wa kweli.(Tudai katiba bora kwanza)Mengine mtayapewa kwa ziada.

  Like

Leave a Reply

Fill in your details below or click an icon to log in:

WordPress.com Logo

You are commenting using your WordPress.com account. Log Out /  Change )

Google photo

You are commenting using your Google account. Log Out /  Change )

Twitter picture

You are commenting using your Twitter account. Log Out /  Change )

Facebook photo

You are commenting using your Facebook account. Log Out /  Change )

Connecting to %s