OMBI KWA DK. MAGUFULI: NITEUE UBALOZI WA CUBA BILA MSHAHARA

NA SABATHO NYAMSENDA

Mpendwa Rais Magufuli,

Pole kwa majukumu ya ujenzi wa taifa. Tafadhali pokea pongezi zangu za dhati kwa uamuzi wa kufungua ubalozi wa Tanzania nchini Cuba. Huu ni uamuzi wa busara na vizazi vyote vitakukumbuka kwa hili.

Nimeamua kuandika barua ya maombi kwa kuwa, tofauti na nchi zingine ambako nafasi za kidiplomasia huombwa kama kazi, hapa kwetu nafasi hizi ni za uteuzi. Na kwa kuwa mamlaka ya uteuzi yapo mikononi mwako, nimeona niwasilishe ombi langu la kuteuliwa kuishika nafasi hiyo. Sijaomba nafasi hiyo ili nipate mshahara mnono wa kibalozi: nipo tayari kuitumikia nafasi hiyo bila mshahara kwa kipindi chote nitakachoiwakilisha nchi yetu huko Cuba.

Pia, baada ya kumaliza kipindi changu cha utumishi nitaomba nivuliwe hadhi ya ubalozi ili nibaki raia wa kawaida. Hii yote ni kuthibitisha kuwa sijaomba nafasi hiyo kwa ajili ya kupata fedha na hadhi. Nimeomba kwa ajili ya kuitumikia nchi yetu katika nafasi ambayo naamini ni nyeti na ikitumiwa vizuri inaweza kutusaidia kuikomboa nchi yetu na watu wake.

Ninaamini kuwa ninavyo vigezo vya kitaaluma vya kuitumikia nafasi hiyo. Shahada zangu mbili za mwanzo zote nimezifanya katika mahusiano ya kimataifa (international relations), na tafiti zangu za kitaaluma zimejikita katika siasa uchumi (political economy). Mahusiano ya kimataifa yaliyojikita katika siasa uchumi humwezesha mwanazuoni kuzifahamu nguvu za kitabaka zinavyofanya kazi katika uwanda wa kidunia ili hatimaye aweze kuchukua upande. Kwangu mie, upande niliochagua ni wa watu wanaonyonywa na kuonewa ndani ya mfumo uliotawaliwa na mabeberu.

Ndio maana, ulipotangaza vita ya uchumi ili kuokoa rasilimali zetu, mie nilikuwa kati ya watu wa mwanzo kukuunga mkono. Sikukuunga mkono kikasuku, niliona uwezekano wa kuchukua hatua za kimapinduzi na ndio maana nilitaka uende mbali zaidi kwa kutaifisha migodi yote na kuiweka chini ya kampuni za serikali.

Japo serikali yako haikuweza kufanya hivyo, lakini imeweka jiwe la msingi kupitia sheria mpya zinazosimika haki na mamlaka ya kudumu ya Watanzania juu ya rasilimali na utajiri asilia (permanent sovereignty on natural wealth and resources) unaopatikana nchini mwao. Hilo ni jiwe la msingi katika mapambano, ambalo juu yake tutapaswa kujenga uchumi unaojitegemea na kumilikiwa na walio wengi.

Halikadhalika, kila mara unapotangaza kutwaa mashamba makubwa ya mabepari na kuyagawa kwa wananchi wanyonge, mie huwa nakuunga mkono na hushauri uende mbali zaidi kwa kufanya mageuzi makubwa ya ardhi (land reform) ambayo yataweka ardhi yote katika umiliki na udhibiti wa wazalishaji wadogo, ambao kwa mtazamo wangu, ndio tunaopaswa kuwatazama kama wawekezaji. Cuba ilifanya hivyo baada ya mapinduzi ya mwaka 1959. Vietnam na China zimefanya hivyo na ndio maana zimeweza kupiga hatua kubwa sana katika maendeleo.

Rais wangu, wapo wanaokudhihaki kwa uamuzi wako wa kutoa elimu bure kwa ngazi msingi na sekondari. Mie sio mmoja wao. Naunga mkono uamuzi huo, japo ningependa uende mbali zaidi kwa kutoa elimu bila malipo hadi ngazi ya chuo kikuu. Tena natamani elimu yenyewe inayotolewa iwe ni elimu ya ukombozi, yenye kuwajengea wanafunzi chachu ya kufikiri, kudadisi na kuhoji na yenye kuwafumbua macho juu ya udhalimu wa kitabaka uliomo katika jamii zetu, ili hatimae waweze kuitumia elimu yao kwa manufaa ya wanyonge. Madktari wa Cuba wanafanya hivyo na wamesambaa duniani kote wakitumia taaluma zao za tiba kuyaokoa maisha ya wanyonge na kuleta matumaini.

Wapo wengi wasiokubaliana na uamuzi wako wa kuwaruhusu wamachinga wafanye shughuli zao katikati ya jiji bila bughudha. Mimi nakuunga mkono. Kila mara huisikiliza hotuba yako ya jijini Mwanza mwaka 2016 ambapo kwa mara ya kwanza uliungana na wamachinga kupinga kuondolewa katikati ya jiji, na ukatangaza haki ya wavujajasho kufanya shughuli zao katikati ya jiji kuwa ni haki ya msingi ambayo haipaswi kukiukwa na mamlaka yoyote ile, na pale inapokiukwa basi wavujajasho wanapaswa kuipinga mamlaka hiyo. Watawala serikalini hawakukuelewa, wakapotosha kauli yako na kuendelea kuwabughudhi wamachinga. Hukukubali: ukaingilia kati na kutoa tamko kali la kuwaonya watawala wote wanaokaidi agizo lako, na kuwatamkia kuwa wasiopenda kuwaona wamachinga katika maeneo wanayoyaongoza basi wajiuzulu mara moja!

Niseme nini, ndugu Rais? Niseme kuhusu uamuzi wako wa kuiondoa Tanzania katika mikataba ya kinyonyaji ya kimataifa, ukiwemo ule wa EPA (Economic Partnership Agreement)? Au nizungumze kuhusu maamuzi ya kimya kimya ya kuiondoa Tanzania katika mikataba yenye masharti ya kinyonyaji inayoletwa na nchi za magharibi (Bilateral Investment Treaties – BIT), ukiwemo ule wa Tanzania na Uholanzi (Dutch-Tanzania BIT) ambao serikali imeamua kuusitisha?

Hatua zote hizo nilizozitaja, ndugu Rais, ni hatua zinazohitaji kuungwa mkono, kuimarishwa kiitikadi na kupewa mshikamano wa kimataifa. Cuba ni mojawapo ya nchi iliyoimarisha hatua hizo. Balozi wa Tanzania nchini Cuba hapaswi tu kuishia kuhudhuria dhifa za kidiplomasia na kutafuta wawekezaji.

Balozi huyo atapaswa aelewe kuwa Cuba hakuna wawekezaji wa kuja hapa nchini. Waziri Mkuu Kassim Majaliwa alipotembelea Cuba mwaka 2017, alivutiwa na namna Wa-Cuba wanavyoendesha viwanda vya sukari hata akatoa ombi waje wawekeze Tanzania. Kwanza, alijibiwa kuwa viwanda hivyo siyo vya watu binafsi bali vinamilikiwa ama na serikali ama vyama vya ushirika. Pili, aliambiwa kuwa Cuba haina sera ya kunyonya nchi zingine, bali inashirikiana nazo ili ziweze kujitegemea zenyewe. Wa-Cuba walionyesha utayari wa kuleta teknolojia yao hapa nchini, ili sisi wenyewe tujenge na kuvimiliki viwanda hivyo. Sina hakika kama hilo limeshafanyiwa kazi.

Tunao mfano hai wa ushirikiano huo. Pale serikali ya awamu ya nne ilipoanzisha vita dhidi ya malaria kulikuwa na masuluhisho ya aina mbili. La kwanza lilitokea Marekani, ambalo lilikuja kwa njia ya misaada ya vyandarua. Hili halikuwa suluhisho la kudumu, na pia misaada ya Marekani ilikuja na masharti na ilikuwa ni njia ya kupenyeza makampuni ya Marekani yapore rasilimali zetu. Suluhisho la pili lilitokea Cuba, ambayo ilitujengea kiwanda cha kuzalisha dawa ya kuua mazalia ya mbu. Kwa maana nyingine, iwapo tutafanikiwa kuzuia mazalia ya mbu tutakuwa tumefanikiwa kuondoa malaria nchini Tanzania, na hivyo kuua kabisa biashara ya vyandarua na dawa za malaria. Pengine ndiyo maana kiwanda hicho hakikuanza uzalishaji hata baada ya ujenzi wake kukamilika.

Katika sekta ya huduma za jamii, Cuba imepiga hatua ya juu sana. Huduma za jamii (elimu, afya, n.k.) zinatolewa bila malipo ya aina yoyote ile. Ka-nchi kale kasiko na utajiri mwingi kama wetu kanazitumia rasilimali zake chache kwa uangalifu na kwa usawa ili ziboreshe maisha ya wananchi wake. Na kamepata mafanikio ya hali ya juu. Blogu ya Sauti ya Ujamaa ilichapisha makala yenye kichwa, “Haki za Msingi kwa Wote: Tujifunzayo kutoka kwa Fidel Castro na Mapinduzi ya Cuba.” Mwandishi wa makala hiyo, Njuki Githethwa, anabainisha:

“Shirika la Watoto la Umoja wa Mataifa, UNICEF, linaonesha kwamba kati ya mwaka 2008 na 2012, Cuba ilifanikiwa kuwa na 100% ya watu wazima wanaojua kusoma na kuandika, ukilinganisha kiwango hicho na Marekani iliyokuwa na 78%, Kenya 72% na Tanzania 68%.

“Watoto wanaojiandikisha katika shule za msingi nchini Cuba ni 98.4%, USA [Marekani] ni 95.7%, Kenya ni 84%, na Tanzania ni 98.2%.

“Matarajio ya muda wa kuishi nchini Cuba ni miaka 80, USA [Marekani] ni miaka 78, Kenya ni miaka 61, na Tanzania ni miaka 60.9.”

Mwaka 2014, seneta wa Marekani Tom Harkin, alitembelea Cuba na kutamka maneno haya aliporejea Marekani: “Cuba ni nchi maskini lakini takwimu zao za vifo vya watoto wachanga (life expectancy) zipo chini kuliko zetu. Umri wa mtu kuishi (life expectancy) nchini Cuba upo juu kuliko huku kwetu. Inastajaabisha – mfumo wao wa huduma za afya kwa jamii una mafanikio makubwa sana.”

Huyo ni seneta wa Marekani akistaajabu kuhusu mafanikio ya Cuba katika huduma za jamii. Na mafanikio hayo yamepatikana licha ya hujuma za kijasusi na kijeshi, pamoja na vikwazo vya kiuchumi ambavyo Cuba imewekewa na Marekani. Mathalani, iwapo Cuba itanunua kifaa ambacho kina hata asilimia 2 ya teknolojia ya Marekani, basi kampuni iliyoiuzia Cuba kifaa hicho, hata kama ni kampuni ya China, itapewa adhabu kali sana nchini Marekani.

Marekani, ambayo imeshapoteza nguvu za kiuchumi kwa China, imebakiza nguvu za kijesi (military superpower). Na inatumia mabavu hayo ya kijeshi kuvamia nchi maskini, kuwauwa wananchi wasio na hatia, kuchinja watawala wake na kuharibu chumi za nchi hizo. Tofauti na Marekani, Cuba ni taifa lenye nguvu katika upande wa tiba (medical superpower) na inazitumia nguvu hizo kupeleka madaktari na wahudumu wa afya duniani kote ili waokoe maisha ya wananchi wanyonge na kuleta matumaini katika maisha. Cuba haiishii kutuma madktari tu, bali hutoa nafasi kwa vijana kutoka nchi maskini na familia maskini kwenda nchini humo kusomea udaktari bila malipo. Wanapohitimu, huambiwa wakaitumie taaluma yao kuzitumikia jamii za watu maskini duniani kote.

Nchini Cuba hakuna demokrasia ya vyama vingi bali kuna demokrasia ya nguvu ya wavujajasho. Katika makala yake iitwayo “Mapinduzi ya Cuba na Mfumo Mbadala wa Demokrasia” iliyochapishwa na blogu ya Sauti ya Ujamaa tarehe 22 Desemba 2017, Monica Shank anafafanua kuwa Chama cha Kikomunisti cha Cuba, ambacho ndicho chama pekee, sio chama cha siasa bali kiongozi (vanguard) wa vuguvugu la kimapinduzi. Hakisimamishi wagombea katika uchanguzi, bali wagombea huteuliwa kupitia michakato shirikishi inayofanyika kupitia mavuguvugu ya umma (mass organisations) katika maeneo ya kazi na makazi. Shank anaendelea kufafanua:

“Demokrasia ya Cuba ni demokrasia shirikishi. Watu wanashiriki katika maamuzi yanayowahusu katika ngazi zote za serikali. Wacuba wanapiga kura katika uchaguzi kila baada ya miaka miwili na nusu, lakini baada ya hapo wanaendelea kushiriki, ili watu wenyewe wajitawale na kuwadhibiti wawakilishi wao waliowachagua. Mfumo huu ni tofauti kabisa na mfumo wa Kimarekani na mifumo mingi mingine ya demokrasia ya uwakilishi, ambapo ushirikiano wa watu unaishia siku ya kupiga kura.”

“Ni kinyume na sheria kutumia fedha kufanya kampeni… Huu ndio utofauti mkubwa kati ya demokrasia ya Cuba na ya Marekani – Marekani uchaguzi unanunuliwa. Mabilioni ya dola zinatumika kwenye kampeni na kuwashawishi wanasiasa, kwa hiyo pesa ndio inayotawala. Cuba watu wanatawala.” 

Japokuwa yawezekana lisiwe jambo la afya kuachana na vyama vingi hapa kwetu, lakini tunapaswa kujenga mfumo wa kidemokrasia ambao unaenda zaidi ya mashindano ya vyama na chaguzi za miaka mitano. Mfumo huo wa demokrasia unapaswa kuweka nguvu za maamuzi kwa wavujajasho kupitia vyombo shirikishi kama mikutano mikuu ya vijiji na mitaa, pamoja na vyama vya wavujajasho (mass organisations). Katika hilo, tunaweza kujifunza Cuba.

Katika uwanda wa kimataifa, Cuba haijaacha diplomasia ya ukombozi (liberation diplomacy). Bado inaendelea kukemea na kupambana dhidi ya ubeberu, na kuunga mkono vuguvugu la Wapalestina dhidi ya ukaburu wa Wayahudi, kama ambavyo iliwaunga mkono Waafrika dhidi ya utawala wa makaburu na wakoloni huko Kusini mwa Afrika. Marekani inapozidisha hujuma dhidi ya Venezuela na hata kutishia kuivamia kisheshi, Cuba ndiyo imekuwa mstari wa mbele kupinga ubabe huo wa mabeberu na kushirikiana na Venezuela kuwekeza rasilimali zake katika kuboresha maisha ya wanyonge.

Katika bara la Amerika ya Kusini, Cuba imechochea mashirikiano ya kisiasa na kiuchumi yenye lengo la kuzikomboa nchi hizo kutoka katika makucha ya kinyonyaji ya mabeberu. Miongoni mwa mashirikiano hayo ni Alianza Bolivariana par los Pueblos de Nuestra America (ALBA), ambapo nchi za Amerika ya Kusini zinashirikiana na kubadilishana rasilimali na utalamu ili kujiletea maendeleo pasipo kutegemea unyonyaji wa mabeberu. Tulifanya uamuzi sahihi kuikataa EPA na kuzikataa BITs. Lakini kwa nini hatujajenga ALBA yetu ya kutuletea maendeleo kupitia kujitegemea kwa pamoja (collective self-reliance)?

Ndugu Rais, natamani ningesema tena na tena, hata nikuandikie kitabu kizima juu ya mambo ambayo tunapaswa kujifunza kutoka Cuba. Natumai niliyoyaandika hapa yatakusaidia katika tafakuri juu ya ujenzi wa mfumo mbadala katika nchi yetu. Bila ya ujenzi wa mfumo huo mbadala, nachelea kusema kuwa hatua njema zote ulizozichukua zitapotelea hewani. Kama kuna nchi tunayopaswa kuiga mfano wake, basi nchi hiyo ni Cuba. Iwapo mawazo haya yatafaa, nashauri uyaweke kama hadidu rejea kwa mtu utakayemteua balozi wetu nchini Cuba. Awe ni mtu aliyeiva katika itikadi ya ujamaa na anayeyaamini haya kwa dhati.

Nakutakia kila la heri katika utekelezaji wa majukumu yako.

Wasalaam,
Sabatho Nyamsenda,
Mwananchi.

2 comments

  1. Antipas T. S. Massawe · · Reply

    Ni habari njema kwa jamii yetu ya watanzania iliyo na mengi ya kujifunza na kuiga kwa waCuba na waChina.

    Like

  2. Husseinali · · Reply

    Naunga mkono kwa hoja Hirji…Ni Zahir na Rais wetu ni mzalendo…Anajali Tanzania kwanza!
    Cuba imesaidia Tanzania sana na tuwalete watalaamu wao watusaidie zaidi kwenye fani nyingi ambaye wamepiga hatua sana..
    Sina zaidi lakini nakubaliana na Nd Sabatho.
    Hongera…
    Husseinali- DAR es salaam.Tanzania

    Like

Leave a comment

SAUTI YA UJAMAA

Welcome to the Socialist Voice

Discover WordPress

A daily selection of the best content published on WordPress, collected for you by humans who love to read.

The Daily Post

The Art and Craft of Blogging

WordPress.com News

The latest news on WordPress.com and the WordPress community.