PROF SHIVJI: KAZI YA UANAHABARI NI KAZI TAKATIFU

NA PROF ISSA SHIVJI

Kwanza kabisa nawashukuru sana kwa kunipa heshima hii ya kuwa miongoni mwenu kusherehekea fani na tasnia ya habari kwa kupitia wanahabari wenzetu walioshinda tuzo mbalimbali. Na nawashukuru walioshinda tuzo kutupatia “kisingizio” cha kukusanyika hapa na ku-share stori zetu.

Ya pili, nawapongeza na kuwapa pole wanahabari wote kwa kuendelea kutekeleza jukumu lenu muhimu na la kipekee la kuwahabarisha wananchi na umma kila kukicha katika kipindi hiki kigumu, tena kigumu sana.

Ugumu wa kazi yenu unajulikana na upo sio tu katika maeneo yetu ya Afrika Mashariki lakini duniani kote – kutoka Marekani ya Trump mpaka Morocco ya mfalme, na kutoka India ya Modi mpaka Israel ya BIBI, ambaye inaelekea ana ‘ubinamu’ na Sisi wa Misri. Leo hii Misri ya Sisi imekuwa mfano wa kinachoitwa ‘police state’ (dola la kipolisi) kiasi kwamba nionavyo mie popote pale palipo na sheria kandamizi, tunaweza tukapaita kwa jina la Usisi. Na “Usisi” upo katika nchi nyingi tu. Hata hivyo katika mazingira ya “Usisi”, wanahabari wameendelea kufanya kazi zao.

Kama Tamko lenu la Dar es Salaam la Uhuru wa Uhariri na Uwajibikaji linavyosisitiza, uhuru na haki ya kupasha na kupata habari na uhuru wa kujieleza bila hofu na wasiwasi ni wa UMMA na sio wa wanahabari. Nyie kazi yenu ni kuuwezesha tu umma kufurahia haki na uhuru huu. Kwa hivyo, ninadiriki kusema kazi yenu ni kazi takatifu. Na ninasema hivyo kwa dhati kabisa.

Baada ya maneno haya machache ya utangulizi, napenda nigusie jambo moja tu. Mnajua mie ni msomi, mwanazuoni – kwa hivyo ninajikita zaidi kwenye historia, yaani tulikotoka – kuelezea tuko wapi ni kazi yenu kama wanahabari! Hakuna mwalimu mzuri mwingine kuliko historia.

Kosa la ‘Sedition’:

Napenda kuwaelezea kwa muhtasari tu kosa moja la jinai ambalo liko katika majuzuu ya sheria ya nchi nyingi tu, hususan nchi za Dunia ya tatu, ambazo zilirithi sheria zao za jinai kutoka wakoloni.

Kosa mojawapo ni kosa la sedition, Kiswahili chake labda ni kosa la fitina, isipokuwa haileti uzito. Fitina inayozungumziwa katika kosa hili ni fitina dhidi ya utawala ambayo watawala hufananisha uzito wake na usaliti.

Katika nchi za Ulaya na Uingereza kosa la sedition linaitwa kosa la kale – an ancient offence. Chanzo chake ni utawala wa kiimla, wa kifalme, wa karne ya 17. Ingawa kosa hilo liliendelea kuwa katika vitabu vya sheria vya Uingereza mpaka 2009 lilikuwa halitumiki kabisa kwa sababu haliendani na utawala wa kidemokrasia. Mara ya mwisho shitaka la sedition lilipelekwa mahakamani huko Uingereza ilikuwa mnamo 1947 na hata hivyo kesi haikufanikiwa.

Mwaka 2009 Uingereza ilifuta makosa haya kama sedition na criminal libel. Waziri wao wa Sheria, Claire Ward, alisema, na ninanukuu:

“Sedition and seditious and defamatory libel are arcane offences – from a bygone era when freedom of expression wasn’t seen as the right it is today.

“Freedom of speech is now seen as the touchstone of democracy, and the ability of individuals to criticise the state is crucial to maintaining freedom.”

Hata hivyo, haya makosa ya enzi za kale yanaendelea katika nchi zilizotawaliwa na Uingereza.

Katika himaya zake wakoloni waliingiza kosa hilo katika sheria za jinai, yaani Penal Code, kama walivyofanya hapa kwetu.

Kwani, kosa lenyewe linasemaje? Mtu yeyote kwa kitendo au dhamira anaandika au anatangaza au anatamka jambo ambalo linaweza kuudhalalisha, au kuufedhehesha au kuupunguzia heshima utawala au mtawala anatenda kosa la sedition au fitna na anaweza kufungwa.  Mara nyingi sana ukosoaji wa serikali na watawala huchukuliwa kama kuwapunguzia heshima na kwa hivyo kwa mtazamo wao ni kosa la jinai la sedition.

Ndiyo maana, mnamo 1958 Mwalimu Nyerere alipowakosoa Ma-DC wa kikoloni, kwa maneno makali, alishtakiwa kwa kosa la ‘criminal libel’ ambalo linafanana na kosa la sedition. Mwalimu alitiwa hatiani na kupewa adhabu ya kifungo cha miezi sita au faini. Alilipa faini. Baadae alikuja kujuta kutoa faini kwa sababu ilimkosesha raha ya kuitwa PG (Prison Graduate) kama wenzake wapigania uhuru kama akina Kwame Nkrumah na Nnamdi Azikiwe!

Katika sheria ya ‘Newspapers Act, 1976′, ambayo ilipitishwa wakati wa Mwalimu kosa la sedition lilihamishwa kutoka Penal Code na kuwekwa katika Sheria ya Magazeti. Ingawa, kwa kadri ninavyokumbuka mie, haikutumika sana wakati wa Mwalimu – labda haikuwa na haja kwa sababu magazeti yote yalikuwa mali ya Serikali au Chama. (Hizi zilikuwa zama za chama-dola). Nafikiri ilianza kutumika tena katika awamu ya tatu na kuendelea.

Makosa ya jinai kama sedition, criminal libel, na sheria-dada zake zingine za kuthibiti na kuadhibu wakosoaji na kubanabana uhuru wa kujieleza, kwa maoni yangu, yanadhihirisha mtazamo fulani wa uhusiano kati ya mtawala na mtawaliwa.

Katika kesi moja kutoka Canada, [Boucher v The King [1951] 2 D.L.R. 369], Jaji akizungumzia hili kosa la sedition alisema kwamba kuna mitazamo miwili juu ya uhusiano kati ya mtawala na mtawaliwa. Mtazamo mmoja ni kwamba mtawala ni superior, ni bora, na mtawaliwa ni duni, ni mtu wa chini, ni inferior. Mtawala amejaa na busara, anajua na anaelewa kila kitu. Kama ndivyo ilivyo, basi huwezi kumkosoa mtawala hadharani, kwa uwazi, kwa sababu unampunguzia heshima yake. Hata anapokosea, huna budi umelezee kosa lake kwa heshima na taadhima, na faraghani.

Mtazamo mwingine ni kwamba mtawala ni mtumishi wa umma. Kwa kuwa, umma kwa pamoja hawawezi kujitawala na kupanga utawala, basi wanawachagua watumishi wao wachache kwenda kujaza nafasi katika vyombo vya utawala. Kwa kuwa, hao wanabaki kuwa watumishi wa Umma, Umma au mmoja wao, ana haki ya kumkosoa [mtawala] akikosea, na hata kumfukuza na kumchagua mwingine kama kosa au makosa yake ni makubwa. Kama alivyosema huyu Jaji, mtawaliwa akimkosoa mtawala, “He is finding fault with his servant.” Jaji anahitimisha kwa kusema kwamba kunaweza kukawa ukosoaji ambao unahatarisha amani na usalama wa umma au mali za raia au kushawishi matumizi ya nguvu, violence, ambao unaweza ukawa kosa la jinai, lakini hakuna ukosoaji wowote ambao hauhatarishi usalama na amani mara moja – kwa maana ya immediately – unaweza kuhesabiwa kama kosa la jinai. Kwa mantiki hii, hakuna ukosoaji wowote ambao unahitaji kuchukuliwa kama kosa la jinai katika nchi na jamii ya kidemokrasia.

Kwa maoni yangu, haki na uhuru wa kujieleza (freedom of expression) ni kipimo cha kipekee cha kuainisha kama nchi inayohusika ni demokrasi na nchi ya kimaendeleo. Hata kama nchi yenyewe ni maskini, utaelezaje kuwa kuna umaskini kama hakuna uhuru wa kujieleza!

***

Nihitimishe. Ukweli ni kwamba sheria kandamizi kama sedition zipo katika nchi nyingi tu. Ndiyo maana nawapongeza wanahabari kwa sababu wanafanya kazi zao katika mazingira magumu ya kisheria ambazo badala ya kuwalinda zinaendelea kuwatisha na kuwatesa wanahabari.

Heko kwa wanahabari ambao bado wanaendelea kutimiza wajibu wao na kufanya kazi yao takatifu pamoja na kutolea mhanga. Nawashukuru sana, na sina shaka umma pia unawashukuru, kwa hiyo.

Asanteni sana.

Leave a Reply

Fill in your details below or click an icon to log in:

WordPress.com Logo

You are commenting using your WordPress.com account. Log Out /  Change )

Google photo

You are commenting using your Google account. Log Out /  Change )

Twitter picture

You are commenting using your Twitter account. Log Out /  Change )

Facebook photo

You are commenting using your Facebook account. Log Out /  Change )

Connecting to %s

SAUTI YA UJAMAA

Welcome to the Socialist Voice

Discover

A daily selection of the best content published on WordPress, collected for you by humans who love to read.

The Daily Post

The Art and Craft of Blogging

The WordPress.com Blog

The latest news on WordPress.com and the WordPress community.

%d bloggers like this: